Monthly Archives: February 2019

TIMU YA CAVALIYA NA ZAN KWEREKWE WACHUANA KIWANJA CHA MAISARA

Ligi ya vijana mchezo wa kikapu imeendelea katika kiwanja cha maisara kwa kuwakutanisha timu ya cavaliya dhidi ta zan kwerekwe , mchezo ambao umemalizika kwa timu ya cavaliya kwa kushinga vikapu 80 dhidi ya 55.

Zan kwerekwe waliovalia jezi rangi ya ndimu walionekana kuzidiwa toka kota ya mwanzo ya mchezo.

Mara baada ya mchezo kumalizika makocha wa timu zote mbili walizungumza na zbc michezo kuhusina na mchezo huo.

MKURUGENZI WA VIPINDI NA UZALISHAJI WA CLOUDS MEDIA GROUP TANZANIA RUGE MUTAHABA AMERAFIKI DUNIA

Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa clouds media group tanzania ruge mutahaba amerafiki duniani nchini afrika kusini alipokuwa  akipatiwa matibabu ya figo.

Ruge ametoa mchango mkubwa katika tasnia ya habari, burudani, na alikuwa na juhudi za kujenga fikra za maendeleo ya vijana tanzania.

Mutahaba amezaliwa mwaka 1970 huko brooklyn nchini marekani na kupata elimu ya msingi arusha baadae akajiunga na skuli ya sekondari ya forodhani jijini dar es salaam pamoja na pugu.

Baadae alirejea nchini marekani kwa masomo ya elimu ya juu ikiwemo shahada ya uzamili na uzamifu.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa twitter, rais magufuli ametoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki zake wa karibu wakiwemo wasanii wa hapa nchini.

WANANCHI WATOLEWA WITO WA KUYATUNZA MAENEO YENYE VIANZIO VYA VYA MAJI KWA HALI NA MALI

Wakati Wananchi wakitolewa wito wa kuyatunza maeneo yenye vianzio vya vya Maji kwa hali na Mali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafikiria kuyahifadhi Kisheria maeneo yote yenye vianzio hivyo kama ilivyohifadhi Kisheria Misitu Mikuu ya Jozani na Ngezi ili kuilinda  Rasilmali hiyo muhimu kwa ustawi wa Jamii.

Akiahirisha Mkutano wa Kumi na Tatu wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema maeneo ya vianzio vya Maji hayataruhusiwa kufanywa shughuli zozote za Kibinaadamu, hivyo aliwanasihi wale waliojenga katika maeneo hayo wajitayarishe kuondoka kwa hiari yao.

Balozi Seif alisema Serikali imejipanga kupambana na changamoto mbali mbali zinazoikabili Sekta ya Maji ikiwemo upotevu wa Maji unaosababishwa na uchakavu wa Miundombinu, uvamizi wa vianzio vya Maji, mwitiko mdogo wa kuchangia huduma ya Maji pamoja na utumiaji ovyo wa Maji majumbani na Ofisini.

Alisema lengo la Serikali Kuu ni kuongeza Miundombinu  itakayowezesha kujenga nguvu za kuwapatia huduma ya Maji safi na Salama Wananchi wote Unguja na Pemba ambapo usambazaji wa huduma hiyo unakadiriwa ufikie asilimia 97%  kwa maeneo ya Mjini na asilimia 85% Vijijini ifikapo Mwaka 2020.

Aliwaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi washirikiane na Serikali katika kupambana na changamoto hizo ili kuihifadhi Rasilmali hiyo ya Maji inayoonekana kupungua kwa kasi Duniani kutokana na sababu tofauti ikiwemo kuchafuka kwa Mazingira.

Balozi Seif alisema kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Afya Duniani {WHO} ifikapo Mwaka 2025 nusu ya Watu wanaoishi Duniani wapatao zaidi ya Bilioni Nane watakuwa wanaishi kwenye maeneo yenye matatizo ya upatikanaji wa huduma ya Maji.

Akizungumzia Mipango ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali inatayarisha Mkakati Shirikishi wa Kitaifa wa usimamizi wa Taka taka wenye lengo Kuu la kuhakikisha taka zote zinazozalishwa Nchini zinasimamiwa ipasavyo ili Miji yote iwe safi kwa faida ya Kiuchumi, Kimazingira pamoja na Kijamii.

Alisema suala la uchafuzi wa mazingira Nchini hasa utupaji taka na uchimbaji mchanga ovyo bado linaendelea kuleta changamoto kwa Taifa na Wananchi wenyewe katika maeneo mbali mbali Nchini.

Balozi Seif alisema Mamlaka za Serikali za Mitaa zina uwezo wa kusimamia wastani wa asilimia 50% ya Taka zote zinazozalishwa zikiwa na wastani wa Tani Laki 238,700 kwa Mwaka Unguja na Pemba.

Alisema ni jambo la kusikitika kuona taka zinazobakia hutupwa ovyo vichakani badala ya kupelekwa kwenye jaa jipya lililotengenezwa Kitaalamu katika eneo la Kibele.

Alionywa kwamba kuna taarifa zinazoelezea uwepo wa baadhi ya Hoteli za Kitalii hutumia Makampuni ya kukusanya taka taka ambazo kwa tamaa zao za kutaka faida kubwa huishia kuzitupa taka taka hizo kwenye vichaka badala ya eneo maalum lililotengwa na Serikali liliopo Kibele.

Balozi Seif  alizitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzanzia sasa kuhakikisha kwamba Hoteli zote zilizomo kwenye Mamlaka yao zinatumia Makampuni yanayofuata Sheria ya Utunzaji wa Mazingira badala ya kuzitupa ovyo katika Mitaa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi kuacha tabia ya kutupa taka ovyo kwenye mitaro hasa kipindi hichi kinachokaribia kuingia msimu wa Mvua za Masika ambazo wakati mwengine husababisha mafuriko yanayoweza kuleta maafa hapo baadae.

Alisema juhudi za Serikali ilizozichukuwa na inayoendelea kuzichukuwa katika kukabiliana na maafa haziwezi kufanikiwa bila ya mashirikiano ya kina pamoja na Wananchi wake.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali kwa upande wake imejipanga kupambana na maafa yanayoweza kusababishwa na mvua hizo kwa ujenzi wa daraja la Kibonde Mzungu na Mwanakwerekwe sambamba na ujenzi wa Mitaro inayoendelea ya maji ya Mvua katika maeneo mengi ya Mkoa Mjini Magharibi ambayo huonekana kuathirika zaidi wakati wa mvua kubwa zinaponyesha.

Akizungumzia jitihada zinazochukuliwa na Serikali za mapambano dhidi ya vitendo vya Udhalilishaji Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kadhia hiyo bado inaendelea kuwatesa Wanawake na Watoto siku hadi siku na hivi sasa vinaonekana kutokea kwa njia nyengine.

Balozi Seif alisema katika kipindi cha Mwezi Julai hadi Disemba 2018, jumla ya matukio Mia 466 yanayohusu vitendo vya udhalilishaji vikiwemo kubaka 257, kulawiti 56, kuingilia kinyume cha maumbile 8, kutorosha 70, shambulio la aibu 75 yameripotiwa katika vyombo vya Dola.

Alisema kwa vile hali bado ni mbaya katika Jamii aliwashauri na kuwaaidhi Wazazi pamoja na Jamii yote kuwa karibu kwa kufuatilia mienendo ya Watoto wao ili kuweza kujua walipo na wanachofanya muda wote.

Hata hivyo Balozi Seif  aliwakumbusha Masheha na Wananchi Mitaani wanapogundua uwep wa Mtu asiyeeleweka  katika maeneo yao wanapaswa kutoa Taarifa haraka kwenye vyombo husika ili kufuatiliwa na hatimae kujiridhisha na hali halisi ya mazingira ya uwepo wa Mtu huyo.

Alitoa msisitizo kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Viongozi wa Dini, Asasi za Kiraia, Makundi ya Malezi kuendelea kuwaelimisha Wananchi Mitaani katika kusimamia Malezi bora yanayoendana na Mila, Silka na Tamaduni zilizoachwa na Wazee waliopita.

Akigusia Sekta ya Utalii ikiwa ni miongoni mwa muhimili muhimu unaotegemewa na Taifa katika Uchumi wa Nchi Balozi Seif  alisema tukio lolote linaloweza kuhatarisha Sekta hiyo halitavumiliwa na Serikali kwani linaweza kuviza Ustawi wa Jamii kupitia Sekta hiyo.

Alitahadharisha kwamba Serikali inatoa onyo kali kwa wale wanaoendesha vitendo vya uhalifu kwenye Fukwe wanapaswa kuacha mara moja tabia hiyo mbaya inayolitia aibu Taifa kwa wageni wanaoamua kufika Nchini kimatembezi.

“ Hatutamuonea haya Mtu ye yote atakayeendesha vitendo vya uhalifu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake”. Alionya Balozi Seif.

Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwataka Vijana wanaofanya biashara ndogo ndogo kuacha mtindo wa kuwabughudhi Watalii wanapotembea ufukweni kwa kuwalazimisha kununua bidhaa zao hata kama hawazihitaji.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  walijadili Miswada Miwili, kupokea Ripoti za Kamati za Baraza ikiwemo ile ya Kamati Teule ya kuchunguza Majengo ya Skuli 19 za Sekondari  katika Mkutano wa Kumi na Tatu za Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar.

Pia Wajumbe hao walipokea Taarifa ya Serikali inayohusu Hoja ya Mjumbe kuliomba Baraza la Wawakilishi kutoa Maazimio ya kushughulikia kwa haraka tatizo la kuharibika kwa vifaa Tiba vya Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba pamoja na kupokea Muelekeo wa Mpango wa Taifa.

Jumla ya Maswali ya msingi yapatao Mia Moja na Thalathini na Tano na Mia Moja na Kumi na Saba ya nyongeza yaliulizwa na Wajumbe wa Baraza la Waakilishi na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara Tofauti.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar {BLW} limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 08 Mei Mwaka 2019.

SUALA LA KUPAMBANA NA RUSHWA LINA UMUHIMU MKUBWA KATIKA MAENDELEO YA NCHI

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amesema kuwa suala la kupambana na rushwa lina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi wanachama wa jumuiya ya afrika mashariki hasa ikizingatiwa kwamba vitendo hivyo vinazorotesha uchumi na maendeleo.

Dk. Shein ameyasema hayo leo katika ukumbi wa baraza la wawakilishi, chukwani mjini zanzibar wakati akizindua mkutano wa nne wa bunge la afrika mashariki (eala) ambapo kwa mwaka huu unafanyika hapa zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein ameeleza kuwa kuwepo kwa mswada wa rushwa katika mkutano wa bunge hilo mwaka huu kuna umuhimu mkubwa kwani utasaidia katika kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikiathiri sana uchumi na maendeleo ya nchi na wananchi wake.

Amesema kuwa mkutano huo ambao katika miswada yake ambapo miongoni mwao kutakuwepo mswada huo ambao utajadiliwa unakwenda sambamba na juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na nchi wanachama katika kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu wa uchumi.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika jitihada zake za kukomesha vitendo vya rushwa imeunda mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi zanzibar (zaeca) kwa lengo la kushughulikia suala zima la kupambana na rushwa.

Amesema kuwa juhudi hizo zinaendelea kwa mashirikiano ya pamoja na wananchi hatua ambayo imepelekea mamlaka hiyo kuweza kupiga hatua kubwa.

Aliongeza kuwa serikali ya jamhuri ya muungano wa tanzania awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Joseph magufuli imeongeza juhudi zaidi katika kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuweka mikakati mbali mbali.

Alisema kuwa serikali zote mbili ile ya jamhuri ya muungano wa tanzania na ile serikali ya mapinduzi ya zanzibar zimeimarisha usimamizi wa sheria na kuongeza bajeti katika sekta ya sheria sambamba na kuongeza wataalamu ili kusimamia kesi zinazohusiana na rushwa.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa juhudi hizo zitasaidia sana pamoja na zile sheria zitakazotungwa na bunge hilo ambazo zote kwa pamoja zinaweza kufikia lengo lililokusudiwa.

Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza suala zima la kuzingatia umhimu wa maadili na tabia njema katika kutekeleza majukumu ya viongozi hao hasa katika wakati huu ambao teknolojia na mifumo ya maisha imebadilika na baadhi ya wakati hupelekea wabunge kufanya vitendo ambavyo vinahitaji umakini na maamuzi ya busara ili waweze kulinda hadhi yao.

Alisema kwamba inatia moyo kuona kwamba ukanda wa afrika mashariki ni miongoni mwa kanda zinazoongoza katika ukuaji mzuri wa uchumi duniani ambapo katika mwaka wa 2017 uchumi ulikuwa kwa asilimia 4.6 ikilinganishwa na mwaka 2016 ambapo uchumi ulikuwa asilimia 4.4.

Alieleza kuwa hayo ni mafanikio makubwa ambayo yanapaswa kuendelezwa  huku akisisitiza kuwa kutokana na afrika ya mashariki kuwa na zaidi ya watu milioni 162 hali hiyo inapelekea kuwepo kwa soko kubwa la bidha mbali mbali pamoja na huduma muhimu.

Pia, alieleza kuwa afrika mashariki ina ardhi kubwa yenye kilomita za mraba 1.82 milioni ambayo ni vyema rasilimali hiyo ikatumika vizuri ili iweze kuleta tija kwa nchi wanachama.

Vile vile, Rais Dk. Shein alipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na nchi wanachama katika kuhakikisha kwamba jumuiya hiyo inafikia malengo yake hasa katika suala zima la kukuza uchumi, uimarishaji wa utawala bora, uismarishaji wa sheria pamoja na uimarishaji wa amani na utulivu.

Rais Dk. Shein ameeleza kutiwa moyo sana na juhudi za umoja huo za kuimarisha lugha ya kiswahili ambayo hivi sasa imekuwa ni lugha inayounanisha wanachama katika shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

 

Alieleza kuwa zanzibar inathamini sana fursa iliyopewa ya kuwa makamo makuu ya kamisheni ya kiswahili ya afrika mashariki na kuahidi kuwa fursa hiyo itaitumia vizuri ili kuhakikisha malengo yaliokusudiwa yanafikiwa.

Dk. Shein alimuhakikishia spika wa bunge hilo martin ngonga kuwa serikali ya mapinduzi ya zanzibar itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza na kuitangaza lugha ya kiswahili na kufahamisha kwamba kupitia baraza la kiswahili la Zanzibar (bakiza) imekuwa ikiandaa makongamano mbali mbali ya kiwahili ambayo yanajumuisha wataalamu kutoka sehemu mbali mbali duniani.

Alisema kuwa hatua hiyo ina lengo la kukiimarisha na kukuza matumizi sahihi ya kiswahili fasaha kwa kuangalia kwamba Zanzibar ndio chimbuko la kswahili sanifu.

Rais Dk. Shein alisema anaamini kwamba jumuiya hiyo inaweza kuwa eneo muhimu la kiuchumi duniani, hivyo jitihada zaidi zinahitajika katika utekelezaji wa malengo makuu yaliopangwa na jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kushajiisha uekezaji, kuendeleza sekta ya utalii, viwanda, elimu na kutilia mkazo  suala zima la kuongeza ajira na kuimarisha miundombinu.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliitaka jumuiya ya afrika masharik kupitia bunge lake hilo kuchukua jitihada katika kupambana na vitendo mbali mbali vyenye kuathiri uchumi ikiwemo suala zima la utakasishaji wa fedha.

Vile vile, rais dk. Shein alieleza haja ya kuendeleza teknolojia ya habari na mawasiliano huku akiwasisitiza wabunge wa bunge hilo kufanya kazi kwa mashirikiano mazuri na mabunge mwengine ya nchi wanachama ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi mzuri zaidi.

Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kulipongeza bunge hilo kwa kufanya mkutano wake huo hapa zanzibar na yeye kupata fursa kwa mara ya pili kuufungua mkutano huo na kutoa shukurani zake kwa kuweza kukaa pamoja na chombo hicho muhimu cha kutunga sheria.

Rais dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza spika wa bunge hilo kwa  kuchaguliwa kuwa spika wa tano na kuweza kukiongoza chombo hicho huku akiwapongeza wajumbe wote wa bunge hilo kwa kuchaguliwa kukiongoza chombo hicho muhimu katika afrika mashariki.

Pamoja na hayo, alisifu utaratibu wa bunge wa kufanya mikutano katika miji ya nchi wanachama jambo ambalo linapelekea wananch kufahamu majukumu ya chombo hicho ambapo alisema utaratibu huo unaenda sambamba na falsafa ya kuweka umoja na mshikamano kwa watu wa afrika mashariki.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein ameleza kufurahishwa kwake na moja ya miswada ambayo itajadiliwa katika bunge hilo ambayo ni pamoja na mswada wa vita dhidi ya rushwa, masuala ya kijinsia,ulemavu pamoja na mada nyengine zitakazojadili vitendo vya ugaidi vilivyojitokeza nchini kenya.

Nao wabunge hao walitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa heshima kuwa aaliyowapa ya kwenda kuzindua mkutano wao huo na kueleza kufurahishwa kwa kiasi kikubwa na hotua aliyoitoa ambayo imewapa matumaini makubwa.

Nae spika wa bunge hilo martin ngoga alitoa shukurani kwa baraza la wawakilishi Zanzibar pamoja na uongozi wake chini ya spika wa baraza hilo zubeir ali maulid kwa mashirikiano mazuri wanayoyapata ambayo ni chachu katika utekelezaji wao wa kazi.

Aidha, spika huyo alieleza umuhimu wa lugha ya kiswahili katika umoja huo pamoja na wajumbe wa bunge hilo na kueleza mikakati waliyoiweka katika kuhakikisha lugha hiyo inatumika vyema ndani ya bunge hilo pamja na nchi zote za jumuiya hiyo.

Nae spika wa baraza la wawakilishi zubeir ali maulid alieleza mashirikiano mazuri yaliopo kati ya baraza la wawakilishi zanzibar na bunge hilo afrika mashariki na kueleza mafanikio makubwa yaliopatikana katika mashirikiano hayo.

Katika uzinduzi huo wa mkutano wa (eala) ambao unatarajiwa kuwa wa siku 10 moja, viongozi mbali mbali walihudhuria akiemo spika wa bunge hilo martin ngoga, makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi seif ali idd, wenyeviti na mawaziri wa nchi za jumuiya ya nchi za afrika mashariki, spika wa baraza la wawakilishi zanzibar zubeir ali maulid, spika mstaafu pandu ameir kificho, jaji mkuu wa zanzibar omar othman makungu, mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wajumbe wa bunge hilo la afrika mashariki.

 

Powered by Live Score & Live Score App