Recent Posts by asha farouq

CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR (SUZA) KINA DHIMA KUBWA YA KUTOA TAALUMA BORA

Rais wa  zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk. Ali mohamed shein  amesema kuwa chuo kikuu cha taifa cha zanzibar (suza) kina dhima kubwa ya kutoa taaluma bora inayoambatana na kufanya tafiti kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizomo katika jamii.

Dk. Shein ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)aliyasema hayo leo  katika Mahafali ya 14  ya Chuo Kikuu hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo ndani ya Kampasi ya Chuo hicho kiliopo Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kufanya tafiti mbali mbali ni miongoni mwa majukumu ya msingi ya vyuo vikuu jambo ambalo hutoa mchango wa chuo kitaaluma na kupandisha hadhi ya ubora wa chuo chenyewe.

Alikihimiza Chuo Kikuu hicho kiendelee kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Tanzania (COSTECH), ambayo ina wajibu wa kuwawezesha watafiti mbali mbali Tanzania Bara na Zanzibar kufanya tafiti wanazozikusudia.

Dk. Shein aliongeza kuwa Chuo Kikuu hicho kina wajibu wa kutafuta fedha za kufanya tafiti kutoka vyanzo mbali mbali kwani utafiti ni miongoni mwa majukumu ya chuo hicho hasa ikizingatiwa kuwa hakuna maendeleo bila ya utafiti.

Alieleza kuwa utafiti ni ngazi muhimu kwa Wanachuo wa mafunzo ya Uzamili na Uzamivu ambao huwasaidia kuhitimu masomo yao, na kukihimiza chuo hicho kujiandaa kuchapisha majarida ya kitaaluma ambayo wahadhiri na wanachuo wa ngazi ya Uzamili na Uzamivu watapata fursa ya kutuma makala zao zinazotokana na tafiti walizofanya.

Aidha, Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa Chuo hicho kuwaweka sawa baadhi ya wahadhiri wachache ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo pamoja na wafanyakazi wote wanaojaribu kufanya kazi zao kinyume na utaratibu.

Alisema kuwa Wahadhiri, walimu na wafanyakazi wa namna hiyo hawatimizi wajibu wao vizuri na hawachagii maendeleo ya Chuo kwani wafanyakazi wa namna hiyo hawana uzalendo “Si wazalendo na hawastahiki wajigambe kuwa ni wahadhiri wa SUZA. SUZA ni chuo cha watu wenye kuyapenda maendeleo ya viongozi wa baadae”,alisisitiza Dk. Shein.

Alisisitiza kuwa ili mafanikio yapatikane ni vyema kukadumishwa umoja na mshikamano uliopo baina ya wahadhiri, wafanyakazi, wanafunzi na washirika wote wa chuo hicho huku akiwataka kujiepusha na mambo yanayoweza kuleta mifarakano.

Rais Dk. Shein alieleza  mategemeo yake kuwa uongozi wa Wizara ya Afya utaendelea na utaratibu wa kuwaajiri madaktari wazalendo kwa kushirikiana na Tume ya Utumishi Serikalini kwa lengo la kuzimarisha huduma za afya ikiwemo kupunguza tatizo la uhaba wa madaktari katika hopsitali za hapa nchini.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza Wizara hiyo ya Afya kwa kutekeleza agizo lake alilowataka wahakikishe kuwa Hospitali ya Mnazi Mmmoja inatumika kwa kufanya mafunzo ya mazoezi ya madaktari wanaohitimu yaani “Internship” kama ilivyoamuliwa tangu mwaka 1977.

Akitoa nasaha zake Dk. Shein alisisitiza haja ya kuitumia vyema rasilimali ya kuandaa wataalmu wa Shahada za Juu za Lugha ya Kiswahili kwa kuwashirikisha Wazanzibari wanaoishi nchi za nje kuweka mikakati maalum ya kuikuza lugha ya Kiswahili na kubainisha uwezo wa kuwafundisha watu wa mataifa mengine.

Rais Dk. Shein aliwataka wahitimu na wataalamu wa Kiswahili kufanya jitihada ili wajiandae kwa kuzitafuta fursa zilizopo za mahitaji ya wataalamu wa Kiswahili badala ya kukaa na kusubiri Serikali kwuatafutia fursa hizo.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa  Chuo Kikuu hicho kwa mwaka huu wa masomo ambapo Chuo Kitazindua udahili wa programu mpya mbili katika ngazi ya Shahada ambazo ni Shahada ya Sayansi ya Uuguzi (DSc. Nursing) na Shahada ya Sayansi za Kilimo.

Pia, Rais Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake kwa kusikia taarifa za Makamu Mkuu wa Chuo hicho kuwa upo mpango wa kuyafanyia matengenezo makubwa majengo ya Chuo kwa asilimia 75 na kujenga majengo mapya 12 ambapo Serikali imejiandaa kutekeleza Mpango huo ili ufanikiwe.

Dk. Sheinj aliongeza kuwa uongozi wa Chuo ni vyema ukaongeza kasi katika kufuatilia utekelezaji wa Nyaraka za Maelewano (MoU) wanazoingia na Taasisi nyengine kwani chuo hicho kimekwua kikishirikiana na vyuo mbali mbali duniani na kutiliana saini za Maelelewano katika kushirikiana huko.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutimiza wajibu wake ili iweze kuyafanikisha malengo yaliyowekwa kwa kutumia fedha za Bajeti na mipango mengine ambayo imeungwa mkono na nchi marafiki na washirika wa maendeleo.

Aidha, Dk. Shein aliuhimiza uongozi na wanachuo wa Chuo Kikuu hicho kuendeleza masuala ya michezo pamoja na uendelezaji wa midahalo kwani masuala hayo ni muhimu katika vyuo kwa lengo la kuimarisha afya za wanachuo na kuwaongezea maarifa na masuala mbali mbali ya kitaaluma.

Pia, Dk. Shein aliwahimiza wahitimu wa Mahafali hiyo kuzichangamkia fursa zilizoandaliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi na Mipango mengine ili waweze kujiajiri wenyewe na kuwataka kuwa na ndoto kubwa zaidi ya kujiajiri kuliko kusubiri kuajiriwa na Serikalini.

Alieleza kuwa matajiri na watu maarufu zaidi duniani wengi wao ni watu waliojiajiri wenyewe kwa kujishughulisha na biashara, sanaa, michezo na shughuli mbali mbali za ujasiriamali ambapo na wao wakiamua wanaweza kuwa miongoni mwa watu hao.

Katika Mahafali ya mwaka huu ya Chuo Kikuu hicho zipo jumla ya fani za masomo 56 zenye wahitimu 1940 ambapo asilimia 58 ya wahitimu wote ni wanawake na asilimia 42 wanaume ambapo pia kwa mara nyengine tena mwanamke ametokea kuwa mwanafunzi bora.

Nae Makamu Mkuu wa Chuo cha (SUZA), Profesa Idrisa Rai,  alisema kuwa mahafali ya mwaka huu yameandika historia mpya kwa Chuo hicho kwa kutoa wahitimu wa fani ya Udaktari hapa nchini.

Alisema kuwa uanzishaji wa masomo hayo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. Shein alilotowa katika mahafali ya mwaka 2011 kwa lengo la kuhakikisha Zanzibar inajitegemea kuwa wataalamu wa fani hiyo.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dk. Idrissa Muslim Hija kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza hilo, alisema kuwa mahafali ya mwaka huu yamepanua wigo kwa kuongeza fani mbili zaidi tofauti na mwaka uliopita.

Dk. Idrissa alitumia fursa hiyo kuwapongeza washirika wa maendeleo kwa juhudi na mchango wao mkubwa katika kukiendeleza Chuo hicho kupitia nyanja tofauti.

Alizitaja taasisi na mashirika hayo kuwa ni pamoja na Milele Foundation, UNICEF, World Bank, NORAD, DANIDA, HUAWEI, Ubalozi wa Uturuki, Serikali ya Watu wa China pamoja na Falme za Kiarabu.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma  aliipongeza Serikali wka juhudi kubwa inazoendelea kuchukua katika kuiendeleza sekta ya elimu nchini, ikiwemo ya Elimu ya Juu.

 

WAZAZI WATAKIWA KUWAPELEKA WATOTO WAO KATIKA VITUO VYA AFYA ILI KUPATIWA CHANJO

Naibu waziri wa afya Mh Harous Said Suleiman amewataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya kwa ajili ya kupatiwa chanjo ya maradhi mbalimbali ili kupunguza vifo vya watoto.

Ametoa kauli hiyo alipozungumza na wandishi wa habari kuelekea madhimisho ya wiki ya chanjo afrika amesema kutokana na taarifa ya shirikisho la afya duniani imethibitisha kuwa chanjo huzuiya zaidi ya vifo milioni tatu kila mwaka.

Amesema lengo kuu la utoaji wa chanjo ni kuokoa maisha juu ya maradhi yanayoweza kuzuilika  na kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo zote ili kuepuka na maradhi.

Mratibu wa chanjo wizara ya afya Yussuf Haji Makame amesema Zanzibar imeweza kufanikiwa katika utowaji wa chanjo za watoto nakufikia asilimi 90.

Nae afisa kitengo cha chanjo wizara ya afya Abdulhamid Abdalla amesema chanjo hizo zitatolewa kwa watoto waliochini ya miaka mitano na watoto wa kike wenye umri wa miaka 14 pamoja na watoto ambao hawajakamilisha ratiba ya chanjo za awali.

Uzinduzi wa chanjo hiyo unatarajiwa kufanyia kesho katika skuli ya fujoni wilaya ya kaskazini b ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya chanjo afrika inayoadhimishwa kila ifikapo april 30.

SUALA LA MRUNDIKANO WA MAKONTENA KATIKA BANDARI YA ZANZIBAR LINAFIKIA MWISHO

Kamati teule ya Baraza la Mapinduzi imesema itahakikisha suala la mrundikano wa makontena katika bandari ya Zanzibar linafikia mwisho ili kutoa fursa kwa wafanya biashara na meli za mizigo kuingiza na kushusha mizigo yao bila ya usumbufu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Dr. Sira ubwa mwamboya ameeleza  hayo  baada ya kufanya ziara ya kutembelea bandari ya malindi mjini unguja kuona hali halisi na kusema kuwa tatizo hilo linapunguza kasi ya kuongezeka mapato  na kusababisha baadhi ya meli za mizigo kushusha mizigo bandari za nje ikiwemo bandari ya mombasa.

Amesema bandari ni sehemu moja wapo inayoingiza mapato kwa wingi lakini kutokana na kutofanya kazi ipasavyo ndio inayochangia kupungua kwa mapato hayo.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la bandari Keptein Abdalla Juma Abdalla amesema ufinyu wa eneo la kuweka makontena hayo ndio linachangia kuwepo kwa tatizo hilo.

Baadhi ya wafanyakazi  wameiomba serikali kufikiria eneo jengine la kuweka makontena ili kuondosha usumbufu uliopo, huku wakisisitiza  kuwekewa mazingira mazuri ya upatikanaji wa maposho yao.

Waziri wa fedha na mipango Balozi Mohamed Ramia amewataka wafanyakazi hao kuondosha kasoro ziliopo na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta ufanisi.

Kamati hiyo yenye mawaziri 6 akiwemo balozi Mohammed Ramia, Balozi Amina Salum Ali, Mh Moudlin Kastico, Haji Omar Kheir,Mh Juma Ali Khatib na Dr Sira Ubwa Mamboya, ambapo kamati hiyo imeundwa april 14  mwaka huu baada ya serikali kupokea taarifa ya kamati ya fedha kuhusu suala la makontena bandarini.

 

 

WANANCHI WATAKIWA KUEKA MAZINGIRA SAFI KATIKA MAENEO YAO KIPINDI HICHI CHA MVUA

Mkuu wa  wilaya ya Wete Abeid Juma  Ali amewataka wajumbe wa kamati ya maafa ya wilaya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uwekaji wa mazingira safi katika maeneo yao  kipindi hichi cha mvua ili kujikinga na maradhi ya mripuko .

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wajumbe wa kamati ya maafa ya wilaya hapo ofisini kwake Wete mkoa wa kaskazini pemba.

Amesema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha ni vyema  wananchi kuchukuwa tahadhari  kusafisha maeneo yao pamoja  na kuondoa  miti hatarishi  iliokaribu na makaazi  ambayo inaweza kusababisha  maafa.

aidha amewataka wajumbe hao kuhakikisha kila mmoja anasimamia majukumu yake ipasavyo ili kunusuru maafa yasitoke.

wakichangia katika kikao hicho wajumbe wa kamati  hiyo wamesema watahakikisha wanasimamia ipasavyo kwa kutoa elimu  kwa wananchi juu ya uwekaji wa mazingira salama katika maeneo yao kwa kuziweka taka katika maeneo yaliyosalama.

Mwarab Ali Nuhu afisa afya wilaya, Shaib Itibar afisa wa afya baraza la mji wete  na khamis said afisa elimu wilaya

 

Recent Comments by asha farouq

No comments by asha farouq yet.

Powered by Live Score & Live Score App