BALOZI SEIF AMEIPONGEZA JAMHURI YA CUBA KWA KUMALIZA UCHAGUZI WA BUNGE KWA AMANI NA USALAMA

 

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Jamuhuri ya Cuba kwa kumaliza Uchaguzi wa Bunge salama wa kuwachagua Wajumbe wa Baraza Kuu la Nguvu ya Umma lenye Mamlaka ya kumchagua Rais wa Baraza la Taifa la Nchi hiyo.Amesema uchaguzi huo uliofanyika Mnamo Tarehe 11 Machi, 2018,  ambapo Wajumbe wa Baraza la Taifa la Cuba walimchaguwa Bwana Miguel Diaz –Canel kuwa Rais wa Nchi hiyo aliyekuwa msaidizi wa Kiongozi wa Taifa hilo Bwana Raul Castro ulikuwa na amani na kushuhudiwa na Jumuiya za Kimataifa.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa pongezi hizo wakati akizungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernandes kwenye Makazi yake Jijini  Dar es salaam.Amesema kufuatia kumalizika kwa uchaguzi  huo Tanzania na Cuba zitaendelea kupata wasaa zaidi wa kushirikiana katika masuala na sekta zilizoanzishwa ambazo ana matumaini ya kuendelezwa chini ya Rais huyo Mpya wa Cuba Bwana Magel Diaz – Canel mwenye fikra za watangulizi wake waliolenga kuona ustawi wa Bara la Afrika unaimarika na kukua siku hadi siku.

Akitoa shukrani zake Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernandes alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Cuba itaendelea kuiunga Mkono Tanzania hasa katika masuala ya Elimu na Afya.Profesa Lucas amesema miradi ya pamoja iliyoanzishwa akiutolea mfano ule wa Afya umeanza kutoa sura ya matumaini kufutia baadhi ya Madaktari Wazalendo wa Zanzibar kuendelea na mafunzo yao ya Juu ya Udaktari Nchini Cuba baada ya kumaliza masomo yao Zanzibar chini ya usimamizi wa Wataalamu na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Matantas cha Nchini humo.Kiongozi huyo Mpya wa Taifa la Cuba akiwa wa Tatu tokea Taifa hilo kupata Uhuru wake  alishika wadhifa huo kwa kupata Asilimia 85.65%  baada ya kushinda Viti Mia Sita na Tano.Bwana Miguel Diaz – Canel wa Chama cha Kikoministi anayeshika nafasi hiyo ya Urais katika kipindi cha Miaka Mitano akiendelea hadi Mwaka 2023 amepungukiwa na Viti 7 ikilinganishwa na Uchaguzi uliopita wa Mwaka 2013 ambapo mshindi aliibuka na Viti 612.Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa salamu za pole kwa Rais wa Cuba Bwama Miguel Diaz – Canel kupitia Balozi wa Nchi Hiyo Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo kufuatia ajali ya Ndege ya Boeing 737 ya Shirika la Ndege la Cuba { Cubana Airlines }.

Ajali hiyo iliyotokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Havana wa Jose Marti ilisababisha idadi ya Vifo vya Abiria Mia 111 hadi kufikia mapema Wiki hii ambao walikuwemo kwenye Ndege hiyo.Balozi Seif  kupitia Balozi huyo wa Cuba Nchini Tanzania aliwataka Wananchi wa Cuba pamoja na wale wenye jamaa na ndugu zao waliokumbwa na Umauti huo kuwa na moyo wa Subira katika kipindi hichi kizito cha Msiba.Amesema Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla wanaungana na Serikali ya Cuba pamoja na Wananchi wake katika msiba huo uliojumuisha pia Vijana ambao ndio nguvu kazi iliyokuwa ikitegemewa na Taifa hilo.Ndege hiyo ya Abiria ilipata ajali mara baada ya kuruka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jose Marti  katika Mji  Mkuu wa Havana ikielekea Mji wa Holguin ulioko Mashariki mwa Nchi hiyo.Kwa mujibu wa takwimu za Vyombo vya Habari hiyo ni ajali ya Tatu kubwa za Ndege Nchini Cuba tokea mnamo Mwaka 2010.