BALOZI SEIF AMESEMA MMONG’ONYOKO WA MAADILI KUWAKOSESHA AMANI WAZAZI

 

 

Makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi seif ali iddi amesema vitendo vingi vinavyofanyika ndani ya jamii vinavyochangia  mmong’onyoko wa maadili vinaendelea kuwakosesha amani ya roho wazazi walio wengi nchini.

Amesema vitendo vya utumiaji wa dawa za kulevya, ubakaji, ulawiti, unyanyasaji wa wanawake na watoto vinaonyesha wazi kumalizika kwa maadili ya taifa.

Akilifungua kongamano hukusu maadili ya mtanzania kwa wilaya ya mjini lililofanyika katika ukumbi wa sheikh idriss abdulwakili balozi seif ali iddi amesema maadili ya taifa yanaondoka na sehemu yake inachukuliwa na vitendo viovu.

Balozi seif amesema hali iliyopo ya mmong’onyoko wa maadili inayoendelea hivi sasa jamii yenyewe inapaswa iangalie ilipokosea na kutafuta mbinu za haraka za kuirejesha ili kuepuka kuangamia.

Makamu huyo wa pili wa rais ametahadharisha kwamba taifa linalokosa maadili linakuwa sawa na mwili wa mwanaadamu au kiumbe ye yote asiyekuwa na roho.

Akitoa taarifa ya kongamano hilo katibu wa jumuiya ya wazazi wilaya ya mjini bibi salama abass amesema wilaya ya mjini licha ya jitihada  zinazochukuliwa na viongozi wa serikali lakini bado inaendelea kukumbwa na matukio mbali mbali yanayosababishwa na mporomoko wa maadili ya jamii

Akitoa salamu kwenye kongamano hilo naibu katibu mkuu wa ccm zanzibar dr. Juma abdullah saadala  {mabodi} almeukumbusha  uongozi wa jumuiya ya wazazi kuelewa kwamba wana jukumu na dhima kubwa ya kusimamia malezi bora ya vijana ili taifa liwe na wafuasi wenye maadili na nidhamu iliyotukuka.

Kongamano hilo la mmong’onyoko wa maadili ya mtanzania kwa wilaya ya mjini pamoja na mambo mengine limejadili mada nne ambazo ni pamoja na muelekeo wa mapambano dhidi ya mporomoko wa maadili, dawa za kulevya pamoja na ukimwi.