DK. SHEIN AMEELEZA KUWA ZANZIBAR IKO VIZURI KATIKA UKUSANYAJI WA MAPATO

 

 

Rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk. Ali mohamed shein ameeleza kuwa zanzibar iko vizuri katika ukusanyaji wa mapato hatua ambayo imesababisha uchumi wake uendelee kuimarika siku hadi siku.Dk. Shein  ameyasema hayo, ikulu mjini zanzibar alipokutana na uongozi wa wizara ya fedha na mipango wakati ilipowasilisha utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2017/2018, na mpango kazi wa utekelezaji kwa mwaka 2018/2019.Dk. Shein ametumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi wa wizara fedha na mipango pamoja na watendaji wake wote kwa juhudi kubwa za ukusanyaji wa mapato na kueleza matumaini yake makubwa aliyonayo kwa wizara hiyo.Hivyo, dk. Shein alisisitiza haja ya kuendelea kuimarisha juhudi hizo za ukusanyaji wa mapato ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.

Amesema ikilinganishwa na miaka ya nyuma kwa kiasi kikubwa zanzibar imepunguza kuwatumia wataalamu wa nje katika kuendesha miradi yake ya maendeleo na kazi nyingi katika wizara za serikali hivi sasa zimekuwa zikifanywa na wataalamu wazalendo hali inayoonesha utofauti mkubwa na nchi nyingi za bara la afrika.Rais dk. Shein ametoa wito kwa wizara ya fedha na mipango kutonyamaza kimya kwani  mapato ya zanzibar yameimarika hivyo, ipo haja kwa wananchi kuyajua mafanikio hayo sambamba na mikakati iliyowekwa na serikali katika kuhakikisha mapato yake yanaimarika.Nae katibu mkuu kiongozi na katibu wa baraza la mapinduzi dk. Abdulhamid yahya mzee aliupongeza uwasilishaji mpango kazi na utekelezaji wake uliofanywa na wizara hiyo na kusisitiza haja ya usimamizi wa majuku yao pamoja na kuwasimamia watendaji walio chini yao ili kuepuka udhoroteshwaji wa malengo yaliokusudiwa. Mshauri wa rais ushirikiano wa kimataifa na uchumi balozi mohamed ramia abdiwawa kwa upande wake ameeleza haja ya kutoa taarifa kwa wananchi juu ya mafanikio yaliopatikana ikiwa ni pamoja na kuiletea heshima kubwa zanzibar kiuchumi.

Waziri wa wizara ya fedha na mipango dk. Khalid salum mohamed, amesema uchumi wa zanzibar umeendelea kuimarika na wenye kutoa taswira ya matumaini mazuri mwaka hadi mwaka. Alieleza kuwa  kwa mwaka 2017 pato la taifa limeongezeka na kufikia tzs 1,363 bilioni ikiinganishwa na tzs 1,268 bilioni  kwa mwaka 2016.Kwa mujibu wa maelezo ya waziri huyo pato la taifa linamaanisha kuwa ukuaji halisi wa uchumi wa zanzibar umeongezeka kwa kasi ya asilimia 7.5 mwaka 2017 kasi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.8 ya mwaka 2016.Nao uongozi wa wizara hiyo ulieleza kuwa mafanikio yote yaliopatikana nchini yanatokana na uongozi madhubuti na umakini wa rais dk. Shein katika kusimamia na kuiongoza nchi na wananchi wake na kuahidi kuendelea kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa umakini, ari na kasi ya hali ya juu ili uchumi wa zanzibar uzidi kuimarika.