DK. SHEIN AMESIKITISHWA NA MAWAKILI WANAOITUHUMU MAHKAMA

 

Rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk. Ali mohamed shein amesikitishwa na baadhi ya mawakili wanaoituhumu mahkama kutumika kisiasa na kuhoji nje ya utaratibu maamuzi yanayotolewa na vyombo hivyo halali kikatiba.

Dk.Shein ameyasema hayo katika sherehe ya siku ya sheria zanzibar huko katika ukumbi wa baraza la wawakilishi la zamani, mjini zanzibar.

Katika hotuba yake kwa wananchi, Dk. Shein alisema kuwa tabia hiyo si katika maadili, mila, silka na desturi za Mawakili ambao taaluma yao imetukuka na ambao wanatakiwa kuisaidia Mahkama katika kutenda na kutoa haki.

Dk. Shein alisema kuwa jambo la kushangaza zaidi ni pale baadhi ya Mawakili hao kuvaa majoho yao ya kisheria asubuhi na kwenda kutetea wateja wao Mahkamani, ambao wamewatoza kiwango kikubwa cha fedha, wakitambua kuwa Mahkama ndio chombo pekee cha kikatiba cha kutoa haki lakini hugeuka na huvaa fulana za vyama vya siasa na kuaza kuishutumu Mahkama kuwa ni chombo kinachotumika kisiasa.

Alisema kuwa tabia hiyo inayofanywa na baadhi ya Mawakili hao ni kuingilia uhuru wa Mahkama katika kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya utoaji wa haki.

“Naamini kwamba Mheshimiwa Jaji Mkuu, una uwezo wa kuwashughulikia Mawakili wa aina hii, wanaoitia dosari na kuleta taswira mbaya kwa jamii katika chombo hiki cha Mahkama unachokiongoza na ambacho Majaji wake wamepewa kinga ya Kikatiba katika kufanya kazi na kutimiza majukumu yao ya kutoa haki”,alisisitiza Dk. Shein.

Hivyo Dk. Shein alitoa wito kwa Jaji Mkuu wa kuhakikisha kuwa pale anapotumia uwezo na mamlaka yake aliyopewa na Sheria ya Mawakili Sura ya 28, ya kusajili na kutoa vyeti vya kufanya kazi za Uwakili, anatumia uwezo na mamlaka hayo kwa kusajili Mawakili wenye maslahi ya kuitumikia jamii na sio wanaharakati wanaotumia vibaya taaluma yao.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo katika Siku hiyo ya Sheria kutoa pongezi kwa Mahkama kwa kuendelea na kazi ya kusikiliza na kutoa maamuzi ya kesi mbali mbali zinazowasilishwa na wananchi pamoja na Taasisi mbali mbali za Serikali na Binafsi.

Dk. Shein alieleza kuwa ni vyema kila mwaka badala ya kutoa hotuba peke yake ni vyema kukawepo na taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliopitishwa na maagizo yaliotolewa na viongozi mbali mbali katika maadhimisho ya mwaka uliotangulia.

Alisisitiza kuwa suala la kuishi kwa kuzingatia maadili na utii wa sheria ni wajibu wa kila mwananchi na kuwataka viongozi wote kuwa mfano katika utii wa sheria na kuendeleza maadili mema.

Alisema kuwa viongozi wamechaguliwa au kuteuliwa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi hivyo, wanapaswa kufahamu maadili ya kazi kwa mujibu wa nafasi zao na mategemeo ya wananchi na kuwataka kutii miiko ya uongozi na kufuata uadilifu kwa kuacha vitendo vyote viovu na kuwa mfano katika familia.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya Sheria inayosema “SIMAMIA SHERIA NA MAADILI KATIKA UTEKELEZAJI HAKI”, haiwagusi viongozi wa mahkama tu, bali inawagusa viongozi wa Serikali katika ngazi zote na hata katika taasisi binafsi pamoja na wananchi.

Alieleza kuwa bado wananchi hawaridhishwi na kasi ya uendeshaji wa kesi zinazohusu udhalilishaji wa kijinsia pamoja na kuwepo kwa manunguniko na malalamiko katika utendaji kazi katika Mahkama ya Ardhi.

Alisema kuwa licha ya jitihada zote zinazochukuliwa na Serikali za kuimarisha Mahkama ya Ardhi, bado uwezo wake wa kutoa maamuzi kwa kesi zinazowasilishwa uko chini au inakabiliwa na changamoto nyengine zinazohitaji ufumbuzi.

Dk. Shein pia, alieleza kuwepo kwa uakhirishaji wa kesi mara kwa mara katika mahkama hapa nchini kutokana na Mawakili wengi kushindwa kufika mahakamani kutokanan na sababu mbali mbali hali ambayo ikiendelea itachangia kuwepo kwa mrundikano wa kesi zinazo subiri kusikilizwa na kuzorotesha utoaji wa haki.

Nae Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu alieleza kuwa moja ya faida ya utendaji haki kwa wakati ni ile ya kuwaondoshea wadau usumbufu na gharama za kuhudhuria Mahkama mara kwa mara na kwa muda mrefu.

Alisema kuwa haki ikitendeka kwa wakati wadau watapata muda wa kushughulikia shughuli zao binafsi za kijamii au za maendeleo ya Taifa huku akieleza kuwa Mahkama na Sheria ni mali za wananchi na vipo kwa ajili ya kukidhi mahitaji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman nae aliahidi kuendeleza mashirikiano kati ya Wizara hiyo na taasisi zote sheria hapa nchini.

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Said Hassan nae alieleza kuwa dhana ya kusimamia sheria maadili katika utoaji haki ni muhimu katika nchi yoyote inayoheshimu misingi ya kidemokrasia na kusisitiza kuwa usimamizi wa Sheria na maadili katika utoaji haki haikuwahusu watendaji wa Mahkama pekee yao.

Alisisitiza kuwa kwenye utoaji haki haitoshi kwa mtoaji haki kujiridhisha kwamba amefanya haki bali ni lazima jamii husika ione kwamba haki imetendeka.

Mkurugenzi wa Mshtaka Zanzibar Ibrahim Mzee Ibrahim nae alieleza kuwa  ingawa sheria na maadili ni vitu viwili tofauti lakini ni ukweli usiopingika kwamba vitu hivyo vinakwenda sambamba kwa kiasi kikubwa hasa linapokuja suala la utendaji haki.

Alisisitiza kuwa hakuna mashtaka bila ushahidi na wala hakuna hatia bila ya ushahidi na kuitaka jamii isikatae wala isidharau kutoa ushahidi lakini vuile vile ushahidi ukipatikana ni lazima sheria na maadili visimamiwe katika utendaji haki.

Mapema akisoma hotuba Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar  Omar Said Shaaban alisema kuwa kauli mbiu ya maadhimisho hayo inakiri kuwa kuna mmongonyoko wa maadili katika mfumo wa utoaji wa haki.

Sambamba na hayo alieleza kuwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Tume ya Maadili ya viongozi wa ummana Mamlaka ya kupambana na rushwa ni jambo la kupongezwa sana katika vita ya kupambana na rushwa na usimamizi wa maadili.

 

Katika sherehe hizo Dk. Shein alipata fursa ya kuangalia ramani ya jengo la mahkama kuu linalotarajiwa kujengwa huko Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja pamoja na kuzindua kitabu cha sheria cha mwaka 2015.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika sherehe hizo kutoka Serikali ya Mapindzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Balozi Seif Ali Idd, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Jaji Kiongozi, Mwenyekiti wa Baraza la Waakilishi na viongozi wengine.