DK. SHEIN AMEWAAPISHA VIONGOZI ALIOWATEUA HIVI KARIBUNI KUSHIKA NYADHIFA MBALI MBALI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Viongozi walioapishwa na Rais Dk. Shein hivi leo katika hafla iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar ni Majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar ambao ni Khamis Ramadhan Abdalla na Aziza Idd Suwed.
Wengine ni Kubigwa Mashaka Simba ambaye ameapishwa kuwa Katibu wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na George Joseph Kazi aliyeapishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora anayeshughulikia masuala ya Katiba na Sheria. Hafla hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Waziri wa Wizara ya Nchi Osifi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Khamis Juma Maalim, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Wengine ni Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Umma Assa Ahmad Rashid, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Ibrahim Mzee Ibrahim Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali, Wakuu wa Vikosi vya SMZ, Washauri wa Rais wa Zanzibar, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib pamoja na viongozi wengine wa Serikali.