DK. SHEIN AMEWATAKA VIONGOZI WA CCM KUYAELEZA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA NCHINI

 

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi dk. Ali mohamed Shein amewataka viongozi wa ccm kisiwani pemba kuyaeleza mafanikio yaliyopatikana nchini yaliyotekelezwa na serikali  kupitia ilani ya ccm 2015 – 2020.

Dk. Shein ambaye pia ni makamo mwenyekiti wa ccm zanzibar ameyasema hayo huko pemba katika mkutano na wajumbe wa kamati ya siasa wa wilaya   mkoa wa kaskazini pemba.

Katika maelezo yake, dk. Shein amewataka viongozi hao kutembelea miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ile iliyopo kwenye majimbo yao kwani kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao badala ya kusubiri ziara za rais.

Dk. Shein amesema kuwa iwapo viongozi hao watafanya hivyo watakisaidia chama, watawasaidia viongozi na wananchi pamoja na kumsaidia yeye kwani wana wajibu wa kuangalia miradi hiyo na kuonyesha ni jinsi gani wameridhika ama hawakuridhika na baadae kutoa taarifa.

Dk. Shein amewataka viongozi hao kuondosha ukimya kwani wao ndio wenye serikali na wanapaswa kueleza mafanikio hayo kwa wananchi na kutowaacha watu wengine wakaanza kupotosha ukweli na kujipa tamaa kuwa kuna siku watawabadilisha nia wanaccm wa pemba ambao wako imara katika chama chao.

aidha, ameeleza kuwa chama cha siasa ndio kinachotafuta dola hivyo ni lazima viongozi hao washirikiane kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuyaimarisha matawi ya chama chao.

katika hotuba yake hiyo dk. Shein amesema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika kuinua uchumi kwa kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato ambapo sasa serikali inakusanya wastani wa tsh. Bilioni 50 kwa mwezi kutoka wastani wa tsh. Bilioni 13.5 kwa mwezi zilizokuwa zikikusanywa wakati alipoingia madarakani mwaka 2010.

  1. Shein amesema kuwa kutokana na ongezeko hilo la mapato, serikali imepata uwezo wa kuimarisha huduma za jamii zikiwemo elimu, afya, majisafi na salama na amewahakikishia viongozi hao kwamba serikali itatekeleza ahadi yake ya kuongeza kwa asilimia mia (100%) kima cha chini cha mishahara jambo ambalo halijawahi kufanyika duniani kote.

aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa serikali inaendelea kuimarisha sekta zake mbali mbali, hivi sasa imo katika mikakati ya kapaombe ya kuhakikisha kuwa sekta ya habari inaimarika na wananchi wanapata habari kupitia shirika lao la habari la zbc  na tayari limeanza kuonekana na muda mfupi ujao wananchi wa unguja na pemba wataona mabadiliko kutoka matangazo yao

katika suala zima la uchaguzi ndani wa chama hicho, dk. Shein amesema kuwa yeye mwenyewe binafsi pamoja na mwenyekiti wa chama hicho dk. John pombe magufuli watahakikisha rushwa haitokuwa na nafasi katika uongozi wa chama hicho mwaka huu, na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa atakaegundulika kufanya hivyo.

aidha, dk. Shein aliwataka viongozi hao kuweka mbele maslahi ya chama na kujiepusha na makundi na ubinafsi na kusisitiza kuwa watu wanaobainika kuwa na uwezo wa kuongoza na wanachama kujiridhisha, ndio wanaofaa kupewa kuongeza bila ya hila, rushwa au mbinu zozote zisizokubalika katika uchaguzi wa chama hicho mwaka huu.

naibu katibu mkuu wa chama cha mapinduzi zanzibar abdalla juma abdalla amewataka wanaccm kuendelea kushirikiana katika kukiimarisha chama chao kwa lengo la kukipatia ushindi katika uchaguzi badala ya kujitenga kwa kujigawa makundi ndani ya chama.