FUTARI ZIMEONEKANA KUPUNGUA BEI IKILINGWANISHWA NA RAMADHANI YA MWAKA JANA

 

Wakati waislamu nchi wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani, baadhi ya bidhaa za vyakula zinazotumiwa sana katika mwezi huo kwa ajili ya futari zimeonekana kupungua bei ikilingwanishwa na ramadhani ya mwaka jana.

ZBC imetembelea katika soko la Chake Chake na kugundua bidhaa aina ya ndizi ambazo zinapendwa sana katika mwezi huu kupungua bei kwa kufikia shilingi 25,000 kwa ndizi aina ya mtwike mkungu mkubwa wakati mwaka jana uliuzwa shilingi 40,000.

Kwa upande wa ndizi aina ya mkono wa tembo mikungu miwili inapatikana kwa  shilingi 25,000  wakati mwaka jana ziliuzwa katika ya shilingi 25,000 mpaka 30,000. huku bidhaa aina ya muhogo fungu ni shilingi 2,000 na viazi majimbi shilingi 5,000.

Kwa upande wa bidhaa za nafaka ambazo zinapatikana zaidi katika soko la Tibirinzi, nako baadhi zimeonekana kupanda bei ikiwemo njugu mawe ambazo zinauzwa kati ya shilingi 2,500 na 3,500 ,wakati baadhi ya aina za  maharagwe yanayotumiwa sana katika mwezi mtukufu wa ramadhani hakuna katika soko hilo.

Nao walaji wa bidhaa hizo wamewaomba wafanyabishara wasiutumie mwezi mtukufu wa ramadhani kwa kuwakomowa waislamu kwa kupandisha bei za vitu wanavyouza bali wafanyebiashara zao bila ya udanganyifu.

Bidhaa nyengine iliyonaswa na camera ya ZBC ni bidhaa aina ya nazi ambayo bei yake ikiwa ni shilingi 3,000 kwa fungu huku samaki wakionekana wakiwa na bei kubwa.