ISRAEL YAWEKA KAMERA ZA USALAMA KATIKA ENEO TAKATIFU LA JERUSALEM

Israel imeweka kamera mpya za kiusalama katika lango la kuingia eneo tete takatifu la Jerusalem. Kamera hizo zimeonekana leo huku Israel ikisema inafikiria kuhusu suluhisho mbadala wa mashine za kutambua vyuma ambazo ziliwekwa na Israel katika lango la kuingia eneo hilo lenye msikiti wa al-Aqsa wiki iliyopita, baada ya mtu mwenye asili ya kiarabu aliyekuwa na bunduki kuwapiga risasi maafisa wawili wa polisi na kuwaua. Mashine hizo zimepingwa na Wapalestina na kusababisha vurugu ambapo watu kadhaa wameuawa tangu wiki iliyopita wakiwemo Wapalestina watatu. Waislamu eneo hilo walianzisha harakati za kufanya swala ya umma kupinga hatua ya Israel. Mufti Mkuu wa Jerusalem Sheikh Muhammad Hussein ametaka hali irudishwe kama ilivyokuwa mwanzoni. Wakati huohuo jeshi la Israel limesema limefanya oparesheni kadhaa katika Ukingo wa Magharibi na kuwakamata watu 29 wakiwemo wanachama tisa wa kundi la wanamgambo wa Hamas. Operesheni hiyo imejiri baada ya familia moja ya Kiisraeli ya watu watatu kuchomwa kisu hadi kufa.