Jeshi la syria lathibitisha kuukomboa mji wa aleppo

Serikali ya Syria imefanikiwa kurejesha mamlaka yake kikamilifu katika mji wa Aleppo ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minne kufuatia kuondolewa kundi la mwisho la wapiganaji wa makundi ya waasi pamoja na raia. Hatua hiyo inaonyesha kumaliza mapigano yaliyochukua karibu miaka sita na kuiwezesha serikali inayoongozwa na Rais Bashar al-Assad kuwa na mamlaka tena kamili katika mji wa Aleppo ambao ni mji mkubwa uliokuwa ukisifika kwa biashara nchini humo. Tangazo la kukombolewa rasmi kwa mji huo lilitolewa kupitia taarifa ya jeshi la nchi hiyo na Kamanda mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama nchini humo alivipongeza vikosi vya serikali pamoja na washirika wao kwa kufanikisha operesheniya kuukomboa mji huo wa Aleppo.