JESHI LA VENEZUELA LATANGAZA KUMUUNGA MKONO MADURO

https://youtu.be/_Q4TXglzUUw

Jeshi la Venezuela latangaza kumuunga mkono maduro

 

Jeshi la Venezuela limesisitiza liko tiifu kwa Rais Nicolas Maduro likisema litalinda kura yenye utata iliyoitishwa na Rais huyo kufanyika wiki ijayo ya kuchagua baraza maalumu litakaloandika katiba mpya.

Msimamo huo wa Jeshi wa kumuunga mkono Rais Maduro umetangazwa na Waziri wa ulinzi Jenerali Vladimir Padrino Lopez, hiyo ikiwa hatua nyingine ya kupinga vitisho vya Rais wa Marekani Donald Trump vya kuiwekea Venezuela vikwazo vya kiuchumi iwapo kura hiyo ya kuandika katiba mpya itafanyika.

Upinzani nchini humo umepinga mipango ya Maduro kuteua baraza maalumu la kuandika katiba mpya ukisema ni njama ya kiongozi huyo kung’ang’ania madaraka.

Hii leo maandamano makubwa yanatarajiwa kote nchini humo siku nzima kumshinikiza Maduro kuondoka madarakani. Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na Kanisa Katoliki zote zimelaani mipango ya Maduro kuandika katiba mpya inayoonekana hatua ya kudhihirisha udikteta.