JUMLA YA KESI 136 ZA UDHALILISHAJI ZIMERIPOTIWA KUANZIA JANUARI HADI JULAI MWAKA HUU

Waziri wa nchi ofisi ya rais tawala za mikoa serikali za mitaa na idara maalum za smz, mh. Haji omar kheri amesema jumla ya kesi 136 za udhalilishaji zimeripotiwa kuanzia januari hadi julai mwaka huu katika vituo mbali mbali vya unguja na pemba.
Akitoa taarifa ya utekelezaji ya wizara hiyo iliyotolewa na kamati ya baraza la wawakilishi ya sheria, utawala bora na idara maalum ya smz, amesema idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na mwaka jana ambapo zimeripotiwa kesi 101.
Mh haji amesema viongozi wa mikoa na kamati za shehia wamefanya juhudi kubwa ya kuhamasisha wananchi juu ya kuondoa ukimya na kutoa taarifa ya vitendo vya udhalilishaji vinavyotokea hali iliyosaidia kesi nyingi kuripotiwa.
Akisoma maoni ya kamati mwenyekiti wa kamati ya sheria, utawala bora na idara maalum mh. Machano othman said, ameipongeza serikali kwa kuanzisha mpango wa taifa wa kumaliza udhalilishaji na kuitaka wizara kusimamia kikamilifu mpango huo, pamoja na ameshauri kuondoshwa tatizo la vitendea kazi katika ofisi ya mrajis wa vizazi na vifo ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Wakichangia taarifa hiyo wajumbe wa baraza la wawakilishi wameiomba wizara kuendelea kutoa elimu kwa masheha ili waweze kupata uelewa zaidi wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji na kufikia malengo ya serikali ya mapinduzi ya zanzibar katika kuondosha vitendo hivyo nchini