JUMUIYA YA NCHI ZA KIARABU ZIMEIONYA MAREKANI DHIDI YA UAMUZI WAKE WA KUHAMISHIA UBALOZI WAKE

jumuiya ya nchi za kiarabu, palestina na jordan zimeionya marekani dhidi ya uamuzi wake wa kuhamishia ubalozi wake mjini jerusalem mji ambao unagombaniwa kati ya israel na palestina.
jumuiya hiyo ya nchi za kiarabu imesema hatua hiyo inaweza ikakwamisha mazungumzo yoyote ya siku zijazo na pia inaweza ikasababisha kuibuka tena vurugu katika kanda ya mashariki ya kati.
onyo hilo linakuja wakati rais wa marekani donald trump akifikiria kufanya uamuzi wa kuhamisha ubalozi wa marekani kutoka mjini tel aviv hadi jerusalem, hatua ambayo itakuwa inaashiria kuutambua rasmi mji huo wa kale kama mji mkuu wa israel.
mshauri mwandamizi wa rais wa mamlaka ya ndani ya palestina mahmoud abbas amesema kuwa wameionya marekani kuwa kama serikali ya nchi hiyo itathubutu kuitambua jerusalem kama mji mkuu wa israel na kuhamishia ubalozi wa marekani katika mji huo basi hii itakua ni hatua itakayofikisha mwisho wa fursa ya mazungumzo ya amani.
katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu amesema hatua hiyo ya marekani haitasaidia kuleta amani au uthabiti bali itachochea vurugu na pia kunufaisha upande mmoja ambao ni serikali ya israel.