KAMATI YA MAENDELEO YA KIJIJI YAKUTANANA HALMASHAURI YA WILAYA NA WAUGUZI WA AFYA

 

 

kufuatia sakata la mama mjamzito kujifungulia eneo lisilo rasmi katika kituo cha afya unguja ukuu, kamati ya maendeleo ya kijiji hicho imekutana katika kikao cha pamoja na halmashauri ya wilaya ya kati pamoja na wauguzi wa kituo hicho kujadili suala hilo.

jumanne iliyopita mama mmoja mjamzito ambae alifikishwa kituoni hapo kwa ajili ya kujifungua alilazimika kukaa nje ya kituo kwa muda kusubiri huduma baada ya kukuta mlango ukiwa umefungwa na kutokuwepo muuguzi yeyote, kulazimika kujifungulia eneo lisilo salama muda mfupi tu baada ya kuingizwa ndani ya kituo.

katika kikao hicho masuala muhimu yalijadiliwa ikiwemo halmashauri kuamua kuongeza usimamizi wa karibu kwa kituo hicho cha afya kinachotoa huduma za uzazi kwa saa 24, pamoja na kutoa agizo la kutaka nyumba za daktari zikaliwe na watendaji hao ili kuepusha kujitokeza matatizo mengine.

akizungumza katika kikao hicho mkurugenzi wa halmashauri hiyo nd. mohamed salum mohamed pamoja na msimamizi mkuu wa huduma ya mama na mtoto bi radhia mataka wamesema kwa kilichotokea iwe funzo kwa wauguzi na watendaji wengine kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

aidha wanakijiji pamoja na wajumbe wa kamati ya maendeleo wamewasisitiza watendaji katika kituo hicho cha afya kuwajibika ipasavyo na suala hilo wasilichukulie kwa mzaha kwani lisipochukuliwa hatua linaweza kutoa matokeo mabaya baadae huku watendaji hao wakijitetea kwa kilichotokea kuwa ni tatizo la kibinadamu na kuombakusamehewa.

naibu katibu mkuu wizara ya nchi afisi ya rais tawala za mikoa na idara maalum za smz anaeshughulikia tawala za mikoa na serikali za mitaa nd. kai bashiru mbarouk amesema suala lililotokea linahusu maisha ya mtu moja kwa moja, huku akisema serikali inatenga shilingi bilioni tatu kila mwaka kwa ajili ya huduma za uzazi hivyo si vyema juhudi hizo zikapuuzwa.