KAMISHENI YA KUKABILIANA NA MAAFA KUDHIBITI VITENDO VINAVYOHATARISHA USALAMA NA MAISHA YA WATU

Wajumbe wa kamati za shehia mkoa wa kaskazini unguja wameiomba kamisheni ya kukabiliana na maafa kudhibiti vitendo vinavyohatarisha usalama na maisha ya watu zikiwemo ajali zinazoweza kuepukika.
Wakizungumza baada ya kupatiwa elimu ya kujikinga na majanga yanayosababisha maafa, wajumbe hao wamesema kuna baadhi ya madereva na manahodha huweka maslahi yao zaidi na kutojali usalama wa abiria kwa kupakia idadi kubwa kuliko uwezo wa vyombo vyao.
Wamesema hali hiyo si ya kuvumiliwa kwani imekuwa ya muda mrefu kwa usafiri wa baharini na nchi kavu, hivyo taasisi zinazohusika zinapaswa kulipatia ufumbuzi suala hilo linalogharimu maisha ya binaadamu.
Maafisa kutoka kamisheni ya kukabiliana na maafa wameisisitiza jamii kuepuka mazingira hatarishi yanayosababisha maafa ikiwemo ujenzi wa makaazi mabondeni,kukata miti ovyo na kujiepusha na mambo yanayosababisha kutokea maradhi ya mripuko.
Mafunzo hayo ni mfululizo wa elimu ya kujikinga na maafa inayotolewa na kamisheni ya kukabiliana na maafa katika shehia na taasisi mbali mbali.