Kampuni ya Kimataifa Mahindra kuiunga Mkono Zanzibar katika muelekeo wake wa kuimarisha miradi ya maendelelo

 

 

Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi katika utengenezaji wa vyombo vya Moto  ya  Mahindra yenye Makao Makuu yake Mjini New Delhi Nchini India imeamua kuiunga Mkono Zanzibar katika muelekeo wake wa kuimarisha miradi ya maendelelo.

Mkuu wa shughuli za Kimataifa wa Kampuni hiyo Bwana Arvind Mathew alitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha pamoja kati ya Uongozi wa Kampuni yake na Ujumbe wa Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kilichofanyika Makao Makuu ya Kampuni hiyo yaliyopo Mjini New Delhi.

Bwana Arvind Mathew amesema kutokana na kukuwa  kwa Teknolojia ndani ya Kamupuni ya Mahindra, Uongozi wa Taasisi hiyo ya Uhandisi  Nchini India hivi sasa imekusudia kuelekeza nguvu zake katika Mataifa rafiki kwa nia thabiti ya kuona Mataifa hayo hasa yale ya Bara la Afrika
yanakuwa Kiuchumi.

Amesema Mahindra imejipanga kuangalia njia za kusaidia uimarishaji wa Sekta ya Kilimo kupitia  miundombinu ya vifaa vya Kisasa vitakavyoongeza nguvu za uzalishaji kwa kundi kubwa la Wakulima hasa katika mazao ya viungo yenye tija kubwa katika soko la Kitaifa na Kimataifa.

Amesema Wataalamu wa Kampuni ya Mahindra wamekuwa mashahidi katika safari zao za kawaida kwenye Mataifa mbali mbali waliyowekeza miradi yao ya Kiuchumi kuwaona Wakulima wa maeneo hayo wakiendesha shughuli
zao katika mazingira magumu.

Akitoa shukrani kwa niaba ya ujumbe wake Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Seif  alisema ushirikiano wa karibu uliopo kati ya Zanzibar
na Kampuni ya Mahindra umetoa mchango mkubwa katika kuwakomboa
Wananchi na hasa Wakulima.

Amesema zaidi ya silimia 70 ya Wananchi wa Zanzibar walioko Vijijini
katika Visiwa vya Unguja na Pemba wanaendesha maisha yao ya kila siku
kwa kutegemea sekta ya Kilimo.

Wakati huo huo Ujumbe wa Zanzibar ulikutana kwa mazungumzo na
Wawekezaji pamoja na Wafanyabiashara tofauti wa Mji wa New Delhi na
Majimbo jirani yanayouzunguuka Mji huo yaliyofanyika Makao Makuu ya
Shirikisho la Viwanda  la India { CII }.

Katika mazungumao yao Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirikisho hilo
ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Ushauri wa Kimataifa wa CII Bwana K.K
Kapila alisema India na Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa ujumla zimekuwa
na ushirikiano wa karibu wa Kibiashara uliotiwa saini tokea mwaka
1974.
Bwana Kapila alisema ushirikikano huo unaoende;ea kuimarika kila siku
umeibuwa mchango mkubwa wa msaada wa fedha zitakazosaidia uimarishaji
wa huduma za Maji safi na salama katika Mkoa wa Mjini Magharibi
Zanzibar kufuatia ziara ya mwaka jana ya Uongozi wa ngazi ya juu ya
India uliofika Tanzania Mwezi Disemba mwaka 2015.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
alisema Zanzibar imeshafungua milango ya uwekezaji kwa makampuni mbali
mbali ndani na nje ya Nchini tokea miaka ya 90.

Alisema zipo sekta ambazo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeshazijengea miundombinu imara itakayotoa wepesi kwa Taasisi pamoja
na Makampuni yatakayoamuwa kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi Visiwani
Zanziobar.