KIMBUNGA HARVEY KUIPIGA PWANI YA GHUBA YA MAREKANI

 

Zikiwa zimepita siku tano baada ya kimbunga harvey kuipiga pwani ya ghuba ya marekani, kimbunga hicho kimelipiga jimbo la louisiana kwa mara ya pili ambapo jimbo hilo bado lina kumbukumbu ya maafa yaliyosababishwa na kimbunga katrina cha mwaka 2005.

Rais donald trump jana alizuru texas na kujionea mwenyewe madhara na uharibifu mkubwa uliosababishwa na kimbunga hicho.

Trump amesema zoezi la kutoa misaada litakuwa na gharama kubwa, lakini ameahidi kuwa serikali yake itawasaidia watu wa texas kuweza kuyajenga upya maisha yao.

Eneo kubwa la mji wa houston na maeneo mengine katika ukanda wa pwani ya ghuba ya marekani bado yamekumbwa na mafuriko kutokana na kimbunga hicho kilichotokea mwishoni mwa juma lililopita.

Maafisa wa timu za uokozi na vitengo vya dharura wanaendelea kujaribu kuwafikia mamia ya watu waliokwama, huku wengine zaidi ya 17,000 wakiwa wamepelekwa katika makaazi ya dharura kutokana na nyumba zao kuharibiwa.