KONGAMANO KUHUSU UNYANYASAJI WA WANAWAKE NA WATOTO

Mke wa rais wa zanzibar mama mwanamwema shein amesema bado jamii ina wajibu wa kutafuta mbinu na mikakati zaidi ya kuelimisha ubaya wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto.
Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la siku moja kuhusu unyanyasaji wa wanawake na watoto, lililotayarishwa na taasisi ya mwanaharakati bibi siti bint saad amesema vitendo hivyo vimekuwa sugu hali inayotoa taswira mbaya kwa jamii.
Kutokana na hayo, Mama Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Bint Saad kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu wa Saba pamoja na jitihada za taasisi nyengine katika kukabiliana na vitendo hivyo vibaya.

“Tuna wajibu wa kuchukua hatua za haraka kwani wagenga walisema ‘usipoziba ufa, utajenga ukuta’, sote tuache muhali, tuchukue hatua ili tuepuke kujenga ukuta kwani ni dhahiri kuwa vitendo vya udhalilishaji haviwezi kutupelekea kuwa na jamii bora ya waungwana na wastaarabu wenye maadili mema’,alisema Mama Shein.

Aidha, Mama Shein aliitaka jamii kuzilinda haki za watoto na kuwakinga na vitendo vya udhalilishaji kwa kuziimarisha familia kwani familia zisizokuwa imara huvunjika na kusababisha matatizo kwa watoto, hasa kwa kukosa malezi bora na haki zao nyengine.

Alieleza kuwa baadhi ya tafiti zilizofanywa hivi karibuni zinaonesha kuongezeka kwa idadi ya talaka katika jamii sababu ambayo inatajwa kuwa husababisha watoto kukosa ulinzi wa watu wabaya kupata fursa kuwadhalilisha.

Hivyo, Mama Shein aliwataka wanandoa kuendelea kustahamiliana na kuwataka wazee wazidi kuzilinda ndoa za vijana wao na kuwasisitiza umuhimu wa kuvumiliana na kusameheana ili wajukuu wapate malezi bora huku akiwanasihi viongozi wa dini kuelimisha ubaya na atahri za talaka.

Katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji hasa kwa watoto, Mama Shein alisema kuwa ni lazima wazazi wawe mbele katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao ikiwemo elimu na kueleza kusikitishwa kwake kusikia kuwa katika jamii bado kuna wazazi wanaowakatisha masomo watoto wao kwa ajili ya kuolewa.

Pamoja na hayo, Mama Shein aliunga mkono kauli mbiu ya Kongamano hilo inayosema kwamba “Kina mama tumesema unyanyasaji wa kijinsia sasa basi” na kusisitiza mashirikiano ya pamoja katika kuhakikisha malengo ya kongamano hilo yanafikiwa.

Nae Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico alisema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na taasisi zinazoshughulikia masuala ya udhalilishaji wa wanawake na watoto inatekeleza wajibu wake kwa mashirikiano makubwa na taasisi hizo zikiwemo za Serikali, zisizo za Kiserikali pamoja na Mashirika ya Maendeleo.

Waziri Castico alisema kuwa mikakati mbali mbali imekuwa ikitumiwa na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali katika kupambana na tatizo hilo ambapo Wizara yake kwa kushirikiana na Wadau mbali mbali imetunga Sera, Sheria na Miongozo mbali mbali inayosimamia utekelezaji wa mapambano hayo.

Alisema kuwa Serikali katika uongozi wa Rais Dk. Shein haikukaa kimya katika kuhakikisha inatokomeza vitendo hivyo na kwamba hatua na mikakati mbali mbali imewekwa katika kufikia azma ya malengo yaliyowekwa na kueleza kuwa vitendo hivyo vilikuwepo tokea zamani lakini vilikuwa havitolewi taarifa.

Nae Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanaharakati Siti Bint Saad, Nasra Mohammed Hilal alieleza umuhimu wa kushirikiana katika kupiga vita suala hilo na kusisitiza kuwa kongamano hilo ni moja kati ya maagizo na maazimio ya Taasisi yake.

Mapema Mratibu wa Taasisi hiyo Aziza Saleh alisema kuwa Taasisi hiyo inaelewa fika ugumu wa vita hivyo na iko tayari kushirikiana na taasisi zote zenye nia na lengo la kupiga vita suala hilo la udhalilishaji wa kijinsia kwa kupitia kongamano hilo litakalosaidia kujua ukubwa wa suala hilo na pia, litajadili katika kupata njia muwafaka na hatua za kulitokomeza kabisa.

Katika kongamano hilo mada mbali mbali zimetolewa zinazohusiana na suala zima la udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika Kongamano hilo wakiwemo Mawaziri, Manaibu Waziri, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed, Mshauri wa Rais anayeshughulikia masuala ya Maendeleo ya Wazee, Wanawake na Watoto Bi Zainab Omar pamoja na viongozi wengine wa Serikali na vyama vya siasa na washiriki wengineo.