KUBAINI VITENDO VYA UDANGANYIFU KWA WANAFUNZI KATIKA UFANYAJI WA MITIHANI

 

 

Wasimamizi wa mtihani wa taifa wa kidatu cha nne mkoa wa kusini unguja wametakiwa kuwa makini katika usimamizi wa mitihani hiyo ili kuweza kubaini vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kufanywa na wanafunzi katika kipindi chote cha ufanyaji wa mitihani yao.

Kaimu mkuu wa mkoa wa kusini unguja mhe: idrissa kitwana mustafa ametoa kauli hiyo huko ukumbi wa mkutano tc dunga wakati alipokuwa akifungua mafunzo elekezi kwa wasimamizi wa vituo vya mtihani ya taifa ambayo inayotarajiwa kufanyia tarehe 30 mwezi huu nchini kote.

Mhe: kitwana amesema kwa vile wasimamizi wa mithani ndio wahusika wakuu katika kufanikisha vyema zoezi hilo wanapaswa kuzingatia suala zima la uadilifu na kufuata sheria na taratibu walizoekewa ili kuepukana na matatizo mbali mbali yanayoweza kujitokeza.

Aidha amewataka walimu wa sekondari katika skuli mbali mbali za mkoa huo kuendeleza juhudi za kuwasaidia watahiniwa hao katika kuwajengea mazingira mazuri kabla ya mitihani yao ili waweze kuepukana na vitendo vya udanganyifu na badala yake kuweza kukabiliana vyema na mitihani yao jambo ambalo litapeleka kupata matokeo mazuri.

Nae kamanda wa polisi mkoa wa kusini unguja ndugu makarani ahmeid amesema jeshi la polisi mkoani humo limejipanga vyema katika kusimamia ipasavyo mitihani hiyo na halitosita kumchukulia hatua za kisheria msimamizi yeyote atakae kwenda kinyume na taratibu za usimamizi wa mtihani huo.

Akizungumza kwa niaba ya wasimamizi wa mitihani mwalim omar moh’d ali ameahidi kwamba watatekeleza vyema jukumu hilo walilopewa na taifa ili kuona kwamba zoezi hilo linafanikiwa ipasavyo.

Zaidi ya wanafunzi 1200 wa kidato cha nne mkoani humo wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya taifa mwaka huu.