KUIMARIKA UHUSIANO KATI YA URUSI NA ZANZIBAR KUTAZIDISHA JUHUDI ZA KUKUZA UCHUMI

Rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk. Ali mohamed shein amesema kuimarika uhusiano kati ya urusi na zanzibar kutazidisha juhudi za kukuza uchumi hasa katika sekta ya utalii.
dk. Shein amesema hayo katika mazungumzo na balozi wa urusi nchini tanzania yuri fedorovich popov ambapo ameahidi kuzidisha uhusiano huo.
Katika maelezo yake dk. Shein alisema kuwa ipo haja ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano huo uliopo kati ya nchi hizo kwa kutambua kuwa thamani yake ni kubwa katika maendeleo kwa pande zote mbili.

Dk. Shein alisema kuwa urusi ni nchi moja wapo inayotoa watalii wengi duniani ambao sio wengi wanaozitembelea nchi za bara la afrika ikiwemo tanzania, hivyo alisisitiza haja ya mashirikiano ya pamoja kati ya pande mbili hizo katika kuifanyia kazi sekta hiyo ambayo nimuhimukatika kukuza uchumi na maendeleo hapa nchini.

Dk. Shein aliongeza kuwa kurejea huduma za usafiri wa ndege kati ya tanzania na urusi kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma kupitia shirika lake la ndege la “aeroflot”, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuikamarisha sekta ya utalii hapa nchini kwani itasaidia kuleta watalii kutoka nchi hiyo moja kwa moja.

Sambamba na hayo, dk. Shein alimueleza balozi huyo haja ya kuendeleza na kuongeza nafasi za masomo kwa vijana wa zanzibar wanaokwenda nchi hiyo kwa ajili ya kusoma katika kada mbali mbali za elimu ya juu.

Akizungumzia kuhusu sekta ya biashara, dk. Shein alisema kuwa tanzania ikiwemo zanzibar ina historia kubwa katika sekta ya biashara kati yake na urusi hivyo ipo haja kwa hatua hiyo kurejeshwa kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Aidha, dk. Shein aliipongeza serikali ya urusi kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa karibu kati yake na zanzibar na kueleza kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa nchi za mwanzo kufungua ubalozi wake hapa zanzibar mara tu baada ya mapinduzi ya januari 12, mwaka 1964.

Hivyo, dk. Shein aliitilia mkazo rai ya balozi yuri popov ya kuimarisha uhusiano kama ilivyokuwa katika miaka ya 1970 na 1980 ambapo urusi iliimarisha zaidi uhusiano huo na tanzania ikiwemo zanzibar kwani pia, nchi hiyo ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuyatambua mapinduzi ya zanzibar ya januari 12, 1964.

Nae balozi wa urusi katika jamhuri ya muungano wa tanzania yuri fedorovich popov alimuhakikishia dk. Shein kuwa urusi itaendelea kushirikiana na kuiunga mkono zanzibar kwa kutambua uhusiano na ushirikiano mwema wa kihistoria uliopo.

Katika maelezo yake, balozi yuri alieleza kuwa urusi inatambua umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano huo ambao utakuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote mbili.

Kwa upande wa sekta ya utalii, balozi popov alieleza kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha usafiri wa ndege kati ya urusi na tanzania utarejeshwa ili kukuza sekta hiyo ya utalii pamoja na sekta ya biashara na shughuli za uwekezaji.

Alieleza kuwa kwa upande wa sekta nyengine za maendeleo nchi yake itaongeza nguvu zaidi katika kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana katika sekta hizo ili kuimarisha uchumi na maendeleo kwa nchi mbili hizo.

Pamoja na hayo, balozi popov alitumia fursa hiyo kumpongeza rais dk. Shein kwa kuendelea kuwa rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi kwa kipindi cha pili pamoja na kuwapongeza wananchi wa zanzibar huku akiahidi kuwa wananchi wa urusi wataendeleza ushirikiano na ndugu zao wa zanzibar.