KUKOSEKANA KWA NISHATI YA MAFUTA NA UMEME KUNAWEZA KUPUNGUZA UINGIAJI WA WATALII

 

 

Wawekezaji  katika  sekta  ya  utalii wamesema  kukosekana  kwa  nishati  ya  mafuta  na  kukatika  kwa  umeme  wakati  wa  msimu  wa  utalii, kunaweza  kupunguza  kasi  ya  uingiaji  wa  watalii  hapa  nchini.

Wakiwasilisha  matatizo  yanayozikumba  sekta  binafsi  zinazotoa  huduma  kwa  watalii, kwa  kamati  ya  maendeleo  ya  wanawake  habari  na  utalii, wamesema  wageni  walishindwa  kukamilisha  safari  zao  kwa  wakati  kutokana  na  upungufu  wa  nishati  ya  mafuta  wiki  mbili  zilizopita na  kuwaweka  katika  wakati  mgumu  wamiliki  wa  hoteli.

Wawekezaji  hao  pamoja  na  watoa  huduma  wakiwemo  watembezaji  watalii, pia  wamelalamikia  kukatika  kwa  umeme  katika  kipindi  hicho  jambo  linaweza  kupunguza  ukusanyaji  wa mapato  kwa  serikali  na  sekta  binafsi  yatokanayo  na  utalii, hivyo  wamependekeza  kuandaliwa  mazingira  bora  yatakayowavutia  watalii  kuendelea  kutembelea  hapa  nchini..

Akizungumza  katika  kikao  hicho  mwenyekiti  wa  kamati  ya  maendeleo  ya  wanawake  habari  na  utalii, mh.  Ali  suleiman  shihata, amesema  maombi  yao  yatafanyiwa  kazi  ili  kuhakikisha  kuwa  sekta  ya  utalii  inaendelea  kuimarika, na kuwaomba  wawekezaji  kuwawekea  maslahi  bora  wafanyakazi  wao.