KULINDA RASILIMALI YA MISITU NCHINI

 

 

Waziri wa kilimo maliasili mifugo na uvuvi mhe, rashid ali juma ameitaka idara ya misitu na raslimali zisizorejesheka kuwa balihi wa kutoa vibali vya ukataji miti na usafirishaji wa bidhaa zitokanazo na miti kama ni njia ya kulinda rasilimali hiyo hapa nchini.

Amesema kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi mbali mbali ni kubwa sana na endapo itaendelea kuachwa zanzibar itapoteza rasilimali hiyo kwa kipindi kifupi.

Akizungumza katika kilele cha siku ya misitu duniani katika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi kikwajuni mjini zanzibar mhe, rashid amesema ili visiwa vya zanzibar vibakie katika uhalisia wake ipo haja ya kutumia njia mbadala ya kupata nishati badala ya miti.

Amesema vizazi vijavyo vinahitaji kuona na kuitumia rasilimali hiyo ili visije kulaumu wazazi wao kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani ambayo hivi sasa yamepoteza kabisa rasilimali ya misitu.

Naibu waziri wa wizara hiyo mhe, makame ali ussi  amesema lazima juhudi ya kurejesha miti ya asili iliyokwisha potea kama vile mipipili doria ,mikwe na  mizambarau ifanywe sambamba na watu wanaokamatwa wakiharibu misitu wakamatwe na kuadhibiwa.

Mkurugenzi wa idara ya misitu na rasilimali zisizorejesheka ndugu soud mohammed juma amesema tatizo la uharibifu wa misitu lipo katika nchi nyingi ambapo zanzibar imeitumia siku ya misitu duniani kwa kupanda miti katika maeneo mbali mbali.