KUTANGAZA AJIRA ZA MOJA KWA MOJA ZA WALIMU KWA SKULI ZENYE UHABA WA WALIMU

 

Wizara ya elimu na mafunzo ya amali imepanga mkakati wa kutangaza ajira za moja kwa moja za walimu kwa skuli zenye uhaba wa walimu ambazo miongoni mwao zimepata matokeo mabaya katika mitihani iliyopita.

Naibu waziri wa wizara hiyo mh. Mmanga mjengo mjawiri, amesema mkakati huo utahusisha walimu waliokuwa tayari kufanyakazi katika skuli watakazopangiwa ili kuinua maendeleo ya skuli hizo.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi kompyuta na madawati kwa skuli ya matemwe kigomani yaliyotolewa msaada na hoteli ya matemwe bangaloo, ameitolea mfano skuli ya kigomani ambayo matokeo ya mtihani wa mwaka jana si ya kuridhisha na kusema kuwa wizara ya elimu itaifatilia kwa karibu skuli hiyo ili ifanye vyema katika mitihani ijayo.

Mwalimu mkuu wa skuli hiyo silima mcha haji amesema changamoto kubwa ya skuli hiyo ni uhaba wa walimu hasa wa masomo ya sayansi pamoja na tatizo la ucheleweshaji wa kuandikisha wanafunzi kwa wakati hali inayokwamisha utendaji wa skuli hiyo.

Meneja wa hoteli ya matemwe bangaloo ross owen amesema katika kipindi cha mwaka 2016 hoteli hiyo imetumia zaidi ya shilingi milioni mia mbili kwa misaada mbalimbali ya huduma za jamii pamoja na shughuli za biashara na wenyeji wa kijiji hicho huku ikiahidi kuwashawishi wawekezaji wengine kusaidia maendeleo ya kijiji hicho.