KUZIDISHA UHUSIANO KATI YA TANZANIA NA INDONESIA

 

 

Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi dk. Ali mohamed Shein amefanya mazungumzo na makamu wa Rais wa indonesia Muhammad Yusuf kalla ambapo katika mazungumzo hayo viongozi hao wamekubaliana kuzidisha uhusiano kati ya pande hizo mbili katika sekta za maendeleo.

Katika mazungumzo hayo makamo huyo wa rais wa indonesia alisisitiza haja ya kukuza na kuimarisha uhusiano uliopo kati ya tanzania na indonesia na kueleza kuwa kwa upande wa nchi yake utaendelezwa.

Makamo huyo wa rais, bwana kalla, alieleza kuwa nchi yake inathamini sana uhusiano na ushirikiano huo na kueleza kuwa iko tayari kuviunga mkono vipaumbele vyote vilivyowekwa na tanzania ikiwemo zanzibar katika sekta za maendeleo.

Alisisitiza kuwa jumuiya ya nchi zilizopakana na bahari ya hindi (iora), imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuziweka karibu nchi wanachama wake hatua ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano huo kati ya indonesia na jamhuri ya muungano wa tanzania.

Aidha, kiongozi huyo aliongeza kuwa indonesia inatambua kuwa zanzibar ni nchi mshirika miongoni mwa nchi zinazozalisha karafuu kwa wingi duniani, karafuu ambazo zina sifa kimataifa, hivyo azma ya kushirikiana katika sekta ya biashara na kilimo ina umuhimu wake mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa nchi hizo zimefanana kimazingira.

Pamoja na hayo, kiongozi huyo alieleza kuwa katika suala zima la biashara hivi sasa soko kubwa lipo katika nchi za afrika, hivyo kuwepo kwa mashirikiano hayo kutarahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa pande mbili hizo.

Kwa upande wake dk. Shein, alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa indonesia kwa kufanikisha mkutano huo mkubwa kwa mashirikiano ya pamoja kati ya nchi hiyo na nchi wanachama wa jumuiya ya (iora).

Dk. Shein alimueleza makamo huyo wa rais wa indonesia kuwa tanzania inajivunia kwa kiasi kikubwa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo ambao umeasisiwa na viongozi wakuu wa nchi hizo tokea miaka ya sitini na kuahidi kuwa utaendelezwa.

Aidha, dk. Shein alieleza kuwa kutokana na uhusiano na ushirikiano huo mkubwa kuna haja ya kuuendeleza na kuuimarisha kwa lengo la kunufaika kwa pande zote hasa katika sekta za maendeleo, kiuchumi na kijamii.

Dk. Shein alieleza haja ya kuwepo kwa mashirikiano kati ya nchi hiyo na zanzibar hasa katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, biashara na viwanda, uwekezaji, kilimo, usafiri na usafirishaji, miundombinu, uvuvi, mafuta na gesi pamoja na sekta nyengine muhimu.

Katika maelezo yake dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa vipaumbele vikubwa kwa upande wa jamhuri ya muungano wa tanzania ni kuimarisha sekta ya viwanda na juhudi za makususdi zinaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika.

Hivyo, dk. Shein alisisitiza haja ya nchi hiyo kuimarisha mashirikiano na tanzania ikiwemo zanzibar katika kuimarisha sekta ya viwanda pamoja na biashara ambapo kwa upande wa indonesia sekta hizo zimepata maendeleo makubwa na kupiga hatua kubwa.

Akieleza kwa upande wa sekta ya kilimo, dk. Shein alieleza haja ya mashirikiano katika kuimarisha sekta hiyo hasa katika eneo la utafiti na mafunzo katika sekta hiyo sambamba na kuendeleza hatua zilizochukuliwa kwa pamoja na nchi hizo hapo siku za nyuma.

Katika sekta ya mafuta na gesi, dk. Shein alieleza kuwa tanzania inatambua hatua zilizofikiwa na nchi hiyo katika kuimarisha sekta hiyo na kueleza kuwa tanzania iko tayari kupanua wigo wa mafanikio hayo.

Sambamba na hayo, dk. Shein alieleza juhudi zinazochukuliwa katika kuimarisha sekta ya utalii nchini tanzania na kueleza haja ya kukuza ushirikiano katika kuazisha usafiri wa anga kwa kutumia makampuni ya ndege kati ya nchi mbili hizo.

Pamoja na hayo, dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia uchumi wa zanzibar kwa kiasi kikubwa na ndio sababu sekta hiyo imepewa kipaumbele katika dira ya 2020.

Dk. Shein anatarajiwa kurejea nchini kesho tarehe (9 machi, 2017) baada ya kumaliza mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi na serikali wa jumuiya ya nchi zinazopakana na bahari ya hindi (iora), uliofanyika mjini jakarta indonesia ambapo alimuwakilisha rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania dk. John pombe magufuli.

Mkutano huo wa siku tatu ulianza jumaapili ya tarehe 05 machi na kufikia kilele tarehe 07 machi mwaka huu, mjini jakarta indonesia kwa kuanza na vikao vya mawaziri na wadau wengine kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya nchi zinazopakana na bahari ya hindi (iora) na hatimae mkutano wa viongozi wakuu ulifanyika jana (machi 7, mwaka huu).

Sambamba na mkutano huo, dk. Shein alishiriki katika utiaji saini wa mkataba unaoainisha mikakati, mipango na maazimio yanayolenga kuongeza kasi ya maendeleo ya jumuiya hiyo.

Katika mkutano huo dk. Shein alifuatana na mke wa rais wa zanzibar mama mwanamwema shein, waziri wa biashara, viwanda na masoko, balozi amina salum ali, waziri wa nchi, ofisi ya rais na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi issa, haji ussi gavu, waziri wa kilimo, maliasili, mifugo na uvuvi, hamad rashid mohammed, naibu waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa afika mashariki, dk. Susan alphonce kolimba.

Wengine ni  naibu katibu mkuu wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa afrika mashariki, balozi ramadhani muombwa mwinyi na mshauri wa rais masuala ya ushirikiano wa kimataifa, uchumi na uwekezaji balozi mohamed ramia abdiwawa pamoja na watendaji wengine wa serikali ya jamhuri ya muungano wa tanzania na serikali ya mapinduzi zanzibar.