MAAFISA, WADHAMINI WA TAASISI ZA UMMA KUSIMAMIA NIDHAMU KWA WAFANYAKAZI WANAOWASIMAMIA.

Makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi seif ali iddi amewakumbusha maafisa wadhamini pamoja na viongozi wengine wa taasisi za umma kusimamia nidhamu kwa wafanyakazi wanaowasimamia.
amesema serikali haipendi kuona watendaji wake wanashindwa kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma.
akizungumza na viongozi wa serikali wa mikoa miwili ya pemba hapo katika ukumbi wa makonyo wawi chake chake baada ya kumaliza ziara ya siku mbili kukagua miradi ya maendeleo kisiwani pemba balozi seif ali iddi alionya kwamba nidhamu ya kuingia na kutoka kazini kwa watendaji wa umma kisiwani pemba sio nzuri.
balozi seif amesema maafisa wengi wa taasisi za umma kisiwani pemba wanashindwa kusimamia vyema nidhamu ya uingiaji kazini wa kabla ya honi ya saa moja na nusu asubuhi na utokaji baada ya honi ya saa tisa na nusu jioni.
alisema kitendo hicho kinawapa fursa na kutoa mwanya kwa baadhi ya wafanyakazi wavivu na wale wakorofi kutumia udhaifu huo wa usimamizi mbovu wa baadhi ya maafisa hao na matokeo yake kusababisha uwajibikaji mbovu usioleta tija yoyote ile.
akizungumzia suala la vifaa vya kazi balozi seif aliagiza kuachwa mara moja tabia ya kutumiwa ovyo vyombo vya serikali hasa vile vya moto baada ya saa za kazi kunakooneka kusababisha uchakavu wa haraka wa vyombo hivyo.
alisema chombo cha serikali iwapo hakitakuwa na dharura maalum ya msingi itakayosababisha chombo cha umma kutembea baada ya saa za kazi ni vyema kikalazwa kwa faida ya chombo chenyewe pamoja na kupunguza gharama za matumizi ya mafuta isiyo ya lazima.
mapema akitoa taarifa fupi ya hali ya amani na usalama ndani ya mkoa wa kusini pemba mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambae pia ni mkuu wa mkoa huo mh. mwanajuma majid alisema maisha ya wananchi wa mkoa huo yanaendelea vyema bila ya matukio yoyote ya uvunjifu wa amani katika kipindi hichi.
mh. mwanajuma alisema kilichopo wakati huu ndani ya mkoa kusini pemba ni suala la uhamasishaji wa uchumaji wa zao la karafuu chini ya usimamizi wa kamati maalum { task force } iliyoundwa kusimamia kazi hiyo pamoja na kufuatilia mwenendo mzima wa zoezi hilo.
naye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa kaskazini pemba ambae pia ni mkuu wa mkoa huo mh. omar khamis othman alisema alisema utendaji wa serikali bado una changamoto hasa magari ya wakuu wa wilaya yanayoonekana kuchakaa na kuleta usumbufu kwa watendaji hao wakati wanapofuatilia majukumu yao kwenye maeneo yao ya kazi.
wakitoa michango yao baadhi ya viongozi hao wa serikali wa mikoa miwili ya pemba walitahadharisha ubaya wa majungu unaoonekana kuathiri uwajibikaji kwa taasisi za umma kutokana na baadhi ya watendaji kukumbwa na tuhuma za kadhia za fitina.
walisema serikali inastahiki kuwa makini kwa kufanya uchunguzi wa kina pale inapopelekewa taarifa za makosa yanayodhaniwa kutendwa na baadhi ya kiongozi au mtumishi wa umma vyenginevyo watawavunjika moyo kufanya kazi bidii na uzalendo.
wakizungumzia zoezi la uchumaji wa karafuu maafisa hao wa serikali walisema makali ya sheria iliyowekwa ya zao la karafuu bado ni nyepesi kwa vile inaendelea kutoa mwanya kwa watu wenye tabia ya kufanya magendo ya zao hilo kwa kusafirisha nje ya nchi.