MAFUNZO YANAYOTUMIA MBINU ZA KISASA KUIMARISHA KILIMO NA UFUGAJI

 

Rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mainduzi dr. Ali mohamed shein amesema mafunzo yanayotumia mbinu za kisasa kuimarisha kilimo na ufugaji kwa vijana wanaojiunga na jeshi la kujenga  uchumi yanatoa fursa ya  kujiajiri.

Amesema serikali imeshaandaa mpango  kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi wanapoamua kujikusanya kuanzisha miradi ya kiuchumi  na kupata mikopo hivyo watumie fursa hizo.

Dr. Ali mohamed shein  alieleza hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi seif ali iddi wakati akizindua maadhimisho ya kutimia kwa miaka 40 ya kuanzishwa kwa jeshi la kujenga uchumi zanzibar {jku}.

Sherehe hizo zilizofanyika katika viwanja vya skuli ya sekondari na ufundi ya jku mtoni nje kidogo ya mji wa zanzibar zilitanguliwa na uzinduzi wa bendera ya kikosi hicho cha jeshi la kujenga uchumi zanzibar.

Baadaye  alitembelea maonyesho ya kazi mbali mbali zinazotekelezwa na wapiganaji hao wa jeshi hilo kwenye makambi tofauti ikiwa ni pamoja na miradi ya kilimo, ufugaji, ushoni, huduma za picha, ufundi saramala pamoja na ushoni.

Akizungumza na wapiganaji hao alisema ni jambo la kutia moyo kuona kwamba majukumu ya msingi ya jeshi la kujenga uchumi bado yanatekelezwa na kutafsiriwa kwa vitendo hasa pale wasimamizi na wataalamu wa jeshi hilo wanapoelekeza nguvu zao katika kuwahimiza vijana wao kuimarisha sekta ya kilimo na ufugaji.

 

Alitoa rai kwa viongozi wa majimbo nchini pamoja na vikundi vya ushirika kuitumia fursa ya kwenda kujifunza elimu ya amali na ufundi katika kambi za jku zenye utaalamu mkubwa unaoweza kuwasaidia katika kuongeza ufanisi katika miradi yao.

Rais wa zanzibar aliuhakikishia uongozi na wapiganaji wa jeshi la kujenga uchumi {jku} pamoja na vikosi vyote vya idara maalum kwamba serikali itaendelea kushirikiana na vikosi hivyo ili viwe na nguvu na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Mapema akitoa taarifa za maadhimisho ya kutimia kwa miaka  40 ya kuanzishwa kwa jku kaimu kamanda wa kikosi hicho kanali ali mtumweni ali alisema watumishi wengi wenye nidhamu zilizowapelekea kupanda daraja ndani ya taasisi zao wamepitia na kupata mafunzo ya lazima ya mwaka mmoja ndani ya jku.

Kanal ali mtumweni alisema zaidi ya vijana 55,000  waliomaliza masomo yao tokea kuanzishwa kwa jeshi la kujenga uchumi zanzibar tarehe 3 machi mwaka 1977 ndani ya mikupuo 62  wamepitia jku kwa mujibu wa sheria.

Mapema waziri wa nchi ofisi ya rais tawala za mkikoa, serikali za mitaa na idara maalum za smz mh. Haji omar kheir alisema lengo la kuanzishwa kwa kambi za vijana na baadaye jku ni kuwaunganisha vijana kuwa wamoja bila ya kujali asili au nitikadi zao.

Alisema katika kuona kikosi hicho kinafikia malengo yake wizara ya nchi ofisi ya rais tawala wa mikoa, serikali za mitaa na idara maalum za smz iko katika mpango wa kufanya mapitio ya kuangalia majukumu ya jku  inavyoyatekeleza tokea kuanzishwa kwake mwezi machi mwaka 1977.