MAGUFULI AMEFUNGUA MKUTANO MAALUM WA(CPC)

 

Rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania, dkt. John pombe magufuli, leo tarehe 17 julai, 2018 amefungua mkutano maalum wa majadiliano kati ya chama cha kikomunisti cha china (cpc) na vyama vya siasa vya nchi mbalimbali za afrika unaofanyika kwa siku mbili jijini dar es salaam.

Ujumbe kutoka cpc umeongozwa na waziri wa masuala ya uhusiano wa kimataifa wa cpc mhe. Song tao na afrika imewakilishwa na viongozi kutoka vyama takribani 40 vinavyojumuisha vyama vya ukombozi na ambavyo ni vyama rafiki wa cpc.

Akizungumza katika mkutano huo  rais magufuli ameishukuru cpc na vyama vyote vya afrika kwa kuichagua tanzania kupitia chama cha mapinduzi (ccm) kuwa mwenyeji wa mkutano huo ambao utatoa fursa ya majadiliano ya namna vyama vya siasa vitakavyosaidia serikali zao, kuimarisha sera zake hasa katika masuala ya ukombozi wa kiuchumi na kukuza uhusiano na ushirikiano kati yake na china, ambayo imepata mafanikio makubwa tangu ilipoanza safari ya mageuzi ya kiuchumi miongo minne iliyopita.

Rais magufuli amesema majadiliano hayo yanafanyika wakati ambapo nchi nyingi za afrika (baada ya uhuru) zimepata mafanikio makubwa katika uhusiano wake na china hususan katika masuala ya ulinzi na usalama, biashara, uwekezaji, ujenzi wa miundombinu, kilimo, afya, elimu, sayansi na teknolojia, mazingira, utalii, habari na utamaduni.

Amebainisha kuwa mwaka 2000 baada ya kuanzishwa kwa jukwaa la ushirikianowa china na afrika (focac) ambalo hufanya mikutano yake kila baada ya miaka mitatu, kumekuwa na mafanikio makubwa zaidi ambapo biashara kati ya afrika na china imeongezeka kutoka dola za marekani bilioni 10 hadi zaidi ya dola za marekani bilioni 250 hivi sasa, ambapo uwekezaji wa china barani afrika umeongezeka kutoka dola za marekani milioni 200 hadi kufikia bilioni 35 na hivyo kuifanya china kuwa mshirika mkubwa wa kiuchumi wa afrika.

Aidha, amesema pamoja na china kutoa misaada mingi kwa afrika pia afrika imetoa mchango mkubwa katika kuhakikisha china inapata kiti katika baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Rais magufuli amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ushirikiano huo wa china na afrika, bado kunahitajika  kukuza zaidi uhusiano katika masuala ya kiuchumi kwa kuhakikisha afrika inauza bidhaa nyingi zaidi nchini china, wakati china inaongeza uwekezaji barani afrika hususan katika kilimo, viwanda na madini, na pia kukuza ushirikiano katika ujenzi wa miundombinu ya usafiri na umeme.

Kwa upande wake waziri wa masuala ya uhusiano wa kimataifa wa cpc mhe. Song tao ameishukuru ccm kwa kuandaa mkutano huo mkubwa ambao utasaidia kujadiliana na kubadilishana uzoefu kati ya cpc na vyama vya siasa vya afrika juu ya namna bora ya kuimarisha sera zake ili ziweze kuleta mabadiliko ya kiuchumi kama ambavyo cpc ilifanya.

Mhe. Song tao amebainisha kuwa katika kuimarisha uchumi wa china cpc ilisimamia sera ya “ujamaa na uchumi wa masoko”na ilihakikisha inatilia mkazo watu kufanya kazi na kushiriki katika uzalishaji mali, na kwamba ili kufanikisha hayo ilifanya juhudi kubwa za kuwa na viongozi bora, jambo ambalo imedhamiria kulifanya barani afrika kwa kutoa nafasi 4,000 za mafunzo ya uongozi kwa makada wa vyama vya siasa vya nchi za afrika.