MRADI WA UTAFITI WA KUDHIBITI MARADHI YA KICHOCHO

 

 

Balozi wa china nchini tanzania wang ke ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya mradi wa utafiti wa kudhibiti maradhi ya kichocho zanzibar unaofadhiliwa kwa pamoja kati ya serikali ya china, serikali ya mapinduzi ya zanzibar na shirika la afya duniani.

Amesema licha ya kuwa mradi huo umefikia hatuwa za mwisho za kukamilisha utafiti wa aina mbalimbali za wadudu ambao wanaweza kusababisha maradhi hayo, lakini serikali ya china haitowaacha mkono katika kuhakikisha tatizo hilo linapunguwa na kuondoka kabisa.

Akizungumza mara baada ya kuitembelea ofisi ya kichocho Mkoroshoni Chake Chake  kujionea shughuli zinazofanywa na mradi huo, Balozi WANG amesema lengo la mradi huo ni kuzuwia na kutokomeza  maradhi ya kichocho  Zanzibar na Afrika kwa ujumla.

Amefahamisha kuwa mbali na kupunguza maradhi hayo, pia ni kuwajengea uzowefu  madaktari wazalendo kujuwa sababu za maradhi na namna gani wanaweza kupambana nayo.

Katika hatua nyengine Balozi WANG ameahidi kuwa Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar katika kutowa huduma za afya kwa kuwajengea uzowefu madaktari wazalendo na kuwaletea madaktari mbalimbali.

Naibu waziri wa afya Mh. Harusi Said Suleiman amesema kichocho ni miongoni mwa magonjwa matano yaliyopewa kipaombele kupambana nao kwani, ni ugonjwa hatari ambao unaweza kusababisha ulemavu na vifo vya watoto walioathirika.

Mkuu wa mradi wa kudhibiti kichocho Zanzibar Fatma Kabole amesema miongoni mwa faida zilizopatikana katika mradi huo ni pamoja na madaktari wazalendo kujengewa uwezo na uzowefu wa kujifunza mambo mengi  kutoka kwa walaamu wa Kichina.

Mradi wa kudhibiti kichocho katika kisiwa cha Pemba unatekelezwa katika shehia tatu za majaribio ikiwemo Mtangani, kiuyuminungwini na Wingwi Uwandani.