POLISI IMETUMIA MABOMU YA KUTOA MACHOZI KUWATAWANYA WAFUASI WA UPINZANI

Polisi imetumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa upinzani waliokuwa wakiandamana karibu na mahakama ya juu wakati majaji wa mahakama hiyo wakitoa taarifa kamili kuhusu uamuzi waliochukua kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi uliopita.
Naibu jaji mkuu nchini kenya, philomena mwilu, amesema tume ya uchaguzi, nchini humo ilikataa kuheshimu agizo la mahakama ya juu kufungua mfumo wake wa kompyuta ili ufanyiwe uchunguzi hali iliyopelekea kukubaliwa kwa madai ya upinzani kuwa kulikuwa na kuingiliwa au udukuzi katika mitambo ya tume hiyo.
Katika uamuzi wa tarehe 1 septemba, majaji wakiongozwa na jaji mkuu david maraga walisema kulikuwa na dosari katika zoezi la kuhesabu kura na kuufuta ushindi wa rais uhuru kenyatta aliyetangazwa na tume ya uchaguzi mshindi dhidi ya raila odinga katika uchaguzi wa tarehe nane agosti