SERIKALI KUENDELEA NA JUHUDI ZA KUBUNI MIRADI YA KIUCHUMI

 

 

Serikali ya mkoa wa kusini unguja imesema itaendelea na juhudi za kubuni miradi ya kiuchumi itakayosaidia kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana wa mkoa huo.

Mkuu wa mkoa wa kusini unguja mhe hassan khatib hassan ametoa kauli hiyo wakati akifunga  mafunzo ya miezi sita yanayohusiana na  mradi wa ufugaji nyuki kwa kutumia mbinu za kisasa kwa vijana 37 wa baraza  la vijana wilaya ya kati.

Amesema ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana juhudi za makusudi zinahitajika kwa serikali kuwatafutia njia za kuanzisha miradi itakayoweza kuwakwamua kiuchumi na kuweza kujiajiri wenyewe

Amefahamisha kuwa kwa vile serikali ya mkoa huo inakusudia kulipandisha hadhi zao la asali liwe zao kuu la kibiashara ndani ya mkoa huo hivyo itahakikisha inachukua hatua zinazofaa ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo maalum cha kusarifu asali na mazao mengine ya nyuki  na kuweka soko litakalotambulika ndani na nje ya nchi.

Nao vijana waliopatiwa mafunzo hayo wamesema mbali na kunufaika na  mafunzo hayo lakini bado wanakabiliwa na matatizo ya ukosefu wa ofisi pamoja na uhaba wa vifaa vya kufanyia shughuli zao.