SERIKALI KUSIMAMIA SERA YAKE YA KUTOA ELIMU BURE

 

 

MKE wa Rais wa Zanzibar,Mama Mwanamwema Shein, amesema serikali itaendelea kusimamia sera yake ya kutoa elimu bure, kwa wananchi wa zanzibar, na ni vyema wananchi wakaona umuhimu wa kutumia fursa hiyo kwa kuhakikisha wanasimamia elimu kwa watoto wao.

Mama Shein, aliyasema hayo  wakati akiwahutubia wananchi katika sherehe ya kuwakabidhi vifaa mbali mbali kwa ajili wanafunzi wa Dahalia ya skuli ya sekondari ya Mohamed Juma Pindua  Wilaya ya Mkoani  Kisiwani Pemba, ambapo amewapatia Mashuka, Mablangeti, Sabuni za kufulia na kuogea.

Mama Shein, amesema kuwa serikali kutokana na kujali wananchi wake hivi sasa imeamua kutoa elimu bure kwa ngazi ya msingi na sekondari, jambo ambalo limefanywa kwa makusudi ili kuhakikisha kila Mzanzibari anapata elimu .

Kutokana na hali hiyo, Mama Shein alisema ni vyema kwa Wazanzibari hasa wazazi kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kwa kusimamia elimu ya Watoto wao ikiwa ni hatua itayowawezesha kuitikia wito wa serikali unaowataka kila mtoto alietimiza umri anapatiwa elimu.

Nae Mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Suleiman Iddi,  amewataka wanafunzi hao, kuhakikisha wanasoma kwa bidii, na kuacha kuingia katika mivutano ya kisiasa kwani hivi sasa imeonekana kwa asilimia kubwa kuichafua sekta ya elimu.

Alisema inasikitisha kuona hivi sasa sekta ya elimu hasa katika Vyuo vikuu kutumiwa na Wanasiasa kwa malengo ya kukuza mivutano jambo ambalo tayari limeanza kuonyesha athari yake kwa walimu kushindwa kutimiza wajibu wao wa kutoa elimu na badala yake wamekuwa wakiwaharibu wanafunzi.

Alisema baya zaidi, walimu hao wamekuwa wakitumia nafasi zao vibaya kwa kuwafelisha wanafunzi wanaowaona hawakubaliani na misimamo yao, jambo ambalo ni hatari kwa mustakbali wa sekta ya elimu hapa Zanzibar.

Kutokana na hali hiyo, Mama asha,ameutaka uongozi wa Wizara ya Elimu kuiona hali hiyo na kuhakikisha wanapiga vita vitendo hivyo, ili kuona kila mwenye haki ya kupata elimu anatumia fursa hiyo, kama ilivyokusudiwa na Mzee Abeid Amani Karume.

Mapema Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo Mjawiri, akitoa maelezo yake, alisema ni kweli kumekuwa na hali hiyo na tayari Wizara ya Elimu inakusudia kutoa adhabu kwa wahusika wote baada ya kubaini kuwapo kwa kasoro kadhaa ndani ya sekta hiyo likiwemo suala la siasa katika skuli.

Nae Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo, akitoa maelezo yake, alisema tangu waingie katika kituo hicho wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la uhaba wa huduma ya maji safi na salama na ameiomba serikali kuliangalia suala hilo.

Hata hivyo aliipongeza serikali kwa jitihada ilizozifanya za kuhakikisha inajenga kituo hicho ambacho hivi sasa kimechangia kwa kiasi kikubwa kuinua sekta ya elimu hapa Kisiwani Pemba.