SERIKALI YA MKOA WA KASKAZINI PEMBA IMEFANIKIWA KUZIBAINI EKA 24 ZA MASHAMBA YA SERIKALI

serikali ya mkoa wa kaskazini pemba imefanikiwa kuzibaini eka 24 za mashamba ya serikali yaliyokuwa yakimilikiwa na wananchi kinyume na utaratibu katika shehia ya Kinyasini Wilaya ya Wete.

Mashamba hayo yamepatikana na kurejeshwa serikalini kufuatia ziara ya Mkuu wa Mkoa huo Mh. Omar Khamis Othman ya kuyahakiki na kuyatambua mashamba yote ya serikali yaliyopo katika maeneo mbali mbali ya mkoa huo.

Akizungumza na ZBC akiwa katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa huo Mh. Omar Khamis Othman amesema serikali ya mkoa itaendelea kushirikiana na masheha kuyatafuta na kuyatambua mashamba hayo ili yatumike katika shughuli za uzalishaji.

Mh. Omar ameitumia nafasi hiyo kuigiza wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwamba mashamba yatakayorejeshwa serikali wayaendeleze kwa kuyapanda miti ya biashara na matunda.

Sheha wa shehia ya Kinyasini Raiya Amour Othman na baadhi ya wananchi wakitowa taarifa kuhusu mashamba ya serikali katika eneo hilo walikuwa na maoni tofauti.

Katibu Tawala mkoa huo Ahmed Khalid Abdalla amesemabado mashamba ya serikali yaliyohodhiwa na wananchi na kuyatumia kinyume na utaratibu yako mengi hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kutowa taarifa zinazohusu rasilimali hiyo.