SHUGHULI YA KUWAOKOA WAVULANA WALIOKWAMA PANGONI NCHINI THAILAND YAENDELEA

 

Shughuli ngumu ya kuwaokoa wavulana waliokwama pangoni nchini thailand imeingia siku ya pili leo. Wavulana tisa bado wamekwama pangoni humo. Hapo jana wavulana wanne waliokolewa katika operesheni ya uokozi iliyoongozwa na makundi ya wapigambizi mahiri kabla ya shughuli hiyo kusitishwa. Mvua inayotarajiwa kunyesha ni mojawapo ya adui kwa operesheni ya uokozi, ikitishia kusababisha mafuriko ndani ya pango hilo lililoko kwenye eneo la vilima kaskazini mwa Thailand. Wavulana hao 12 wa timu ya kandanda kwa jina Wild Boars pamoja na kocha wao walikwama kwenye pango hilo liitwalo Tham Luang mnamo Juni 23 pale maji yalipojaa ghafla na kuwazuia kutoka. Ilichukua siku tisa wakitafutwa kabla kugunduliwa wakiwa pangoni. Hapo jana mkuu wa operesheni ya uokozi Narogsak Osottanakorn alisema wavulana wanne waliookolewa wako salama, lakini alitoa maelezo kidogo tu kuhusu hali zao au utambulisho wao.