SMZ ITAENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZILIZOPO KWENYE SEKTA YA ELIMU

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi dk. Ali Mohamed Shein amesema serikali ya mapinduzi ya zanzibar itaendelea kuchukua juhudi kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya elimu hatua kwa hatua.

akizungumza na waalimu wa skuli za sekondari kwa skuli za mikoa mitatu ya unguja, dk. Shein amesema juhudi hizo ni miongoni mwa mikakati ya serikali kuona sekta hiyo inaimarika zaidi.

Katika maelezo yake dk. Shein alieleza kuwa changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiikabili sekta ya elimu tayari zimeshaanza kufanyiwa kazi na serikali anayoiongoza hatua ambayo ni uthibitisho kwamba serikali ina dhamira ya dhati katika kuimarisha sekta ya elimu kwa kuzingatia umuhimu kwa maendeleo.

Alisema kuwa serikali ya mapinduzi ya zanzibar itaendelea kutatua changamoto hizo kwa mujibu wa fedha zilizopo serikalini ili kufanikisha utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya elimu 2016/2020, ilani ya uchaguzi ya ccm 2015-2020, mpango wa mkuza iii  pamoja na mipango mengine ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa.

Dk. Shein alisisitiza kuwa serikali itaweka kipaumbele maalum katika kuimarisha mazingira ya kufanya kazi walimu ili yawe bora zaidi ambapo itahakikisha muundo wa utumishi wa wizara ya elimu unafanyiwa kazi ili kila mfanyakazi wakiwemo walimu wapate stahiki zao kwa mujibu wa sifa za kitaaluma, uzoefu na dhamana zao.

Aidha, dk. Shein alisisitiza haja ya kuimarisha uhusiano baina ya walimu na wazazi ili kuongeza ufanisi katika ufaulu wa wanafunzi hasa ikizingatiwa kuwa hivi sasa katika skuli nyingi kamati za wazee zimepoteza nguvu na hivyo kushindwa kuwaunganisha wazazi na walimu.

Hivyo, dk. Shein alitoa wito kwa uongozi wa skuli kuziimarisha kamati za skuli na hata kuwa na siku za wazazi kwa lengo la kuimarisha uhusiano baina ya wazazi na uongozi wa skuli.

Pia, dk. Shein alisisitiza haja kwa walimu kuwa na mbinu bora za kufundishia na kuwasaidia wanafunzi ikiwa ni pamoja na walimu kujiandaa kabla ya kufundisha na vile vile wawe tayari kujiendeleza kitaaluma na kujifunza kwa wengine wanaofanya vizuri.

Akisisitiza suala la ukaguzi wa skuli na walimu.

Dk. Shein alisema kuwa kwa bahati mbaya katika baadhi ya skuli wapo walimu wachache wanaofanya kazi kwa kuripua ambapo baadhi yao hawakamilishi silibasi na wengine husaza baadhi ya mada na kutilia mkazo masomo ya ziada.

Vile vile, dk. Shein alisema kuwa wapo baadhi ya walimu wanaweka mbele zaidi miradi yao wakati wa kazi na wengine hutumia muda wa kazin kwa porojo za kisiasa na mambo mengine kinyume na wajibu wao wa kusomesha na kufanya hivyo wanakuwa hawasaidii na ni vyema wakachagua kusomesha ama kufanya siasa

Dk. Shein aliitaka idara ya ukaguzi wa elimu kuongeza kasi za ukaguzi katika skuli za serikali na za binafsi ili malengo ya kutoa elimu iliyo bora yaweze kufikiwa kwa ufanisi mkubwa pia, skuli binafsi kuzingatia sheria za utumishi ikiwa ni pamoja kuwapatia mikataba ya kazi watumishi, haki za likizo na stahiki zao pamoja na kuwaajiri walimu wenye sifa.

Pamoja na hayo, dk. Shein  alisisitiza haja ya kuweka mazingira bora katika skuli kwa lengo la kupata matokeo mazuri sambamba na kusisitiza haja kwa walimu kuimarisha michezo katika skuli zao kwani serikali imeanzisha idara ya michezo na utamaduni kwenye wizara ya elimu kwa malengo maalumu

Sambamba na hayo dk. Shein alitoa wito kwa wizara ya elimu kuandaa utaratibu wa kuwazawadia walimu na skuli zinazofanya vizuri zaidi.

Nae waziri wa elimu na mafunzo ya amali riziki pembe juma alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa dk. Shein kwa uwamuzi wake huo wa kuzungumza na walimu wa skuli za sekondari ambao watakuwa mabalozi kwa wenzao.

Mapema katibu mkuu wa wizara hiyo khadija  bakari juma kwa niaba ya walimu na wizara alitumia fursa hiyo kuungana na wananchi kumpongeza dk. Shein kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake katika kipindi cha pili na kueleza mafanikio yaliopatikana katika sekta hiyo ya elimu ikiwa ni pamoja na ongezeko la skuli, madarasa, vitabu, vifaa vyenginevyo.

Katibu mkuu huyo pia, alieleza kuwa wizara hiyo ina kauli mbiu ya “elimu bora kwanza” ikiwa ni msisitizo wa ubora wa elimu kwa wananfunzi wote na kueleza kuwa tayari serikali imeshakamilisha ujenzi wa skuli ya msingi ya mgonjoni, skuli ya sekondari ya mohammed juma pindua ya mkanyageni na skuli ya kwarara ambayo ina kituo cha kurushia matangazo ya redio na televisheni.

 

Aidha, alisema kuwa serikali imeshatangaza zabuni za ujenzi wa skuli tisa za ghorofa zikiwemo skuli tano kwa upande wa unguja na nne kwa upande wa pemba huku akieleza kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi mwengine wa kuendeleza ujenzi wa skuli ya sekondari ya kibuteni umekamilika na mkataba wa ujenzi unatarajiwa kusainiwa hivi karibuni.

Pamoja na hayo, bi khadija alieleza mafanikio zaidi yaliopatikana katika kiwango cha ufaulu katika mitihani ya taifa katika ngazi ya kidato cha pili, kidato ca nnne na kidato cha sita pamoja na ongezeko la wanafunzi waliopatiwa mikopo kupitia bodi ya mikopo ya elimu ya juu zanzibar pamoja na mambo mengineyo katika sekta hiyo ya elimu.

Nao walimu hao walipata nafasi za kutoa risala zao  kwa kila mkoa ndani ya mikoa mitatu ya unguja ambao walieleza mafanikio yaliopatikana katika sekta hiyo ya elimu pamoja na kueleza changamoto zinazowakabili.

Walimu hao pia, walipata fursa ya kutoa michago yao, maoni na ushauri kwa dk. Shein kwa lengo moja la kuimarisha sekta elimu hapa nchini ambapo kwa upande wa walimu wa skuli za binafsi nao walisisitiza haja ya kuwepo mashirikiano ya pamoja.