SMZ KUIMARISHA HUDUMA ZA KIJAMII

 

Serikali ya mapinduzi ya zanzibar itaimarisha huduma za kijamii zikiwemo elimu, afya, makaazi na upatikanaji wa maji safi na salama ikiwa ni vipaumbele vya mpango wa maendeleo mwaka 2017/2018.

Mpango huo utakwenda sambamba na uimarishaji wa miundombinu ya bandari, viwanja vya ndege, nishati pamoja na tafiti zitakazosaidia kutoa maamuzi katika mipango hiyo ya maendeleo.

Makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi seif ali iddi akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo katika baraza la wawakilishi amesema mkazo utawekwa kugharamia mambo hayo kwa kutumia rasilmali zilizopo kwa faida ya wananchi na taifa.

Amesema uchumi wa zanzibar umeimarika kwa asilimia 6 nukta 8 mwaka 2016  kutoka asilimia 6 nukta 5 mwaka 2015.

Kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha na kuleta maafa balozi seif amesema serikali inawasisitiza wananchi kuepuka kujenga katika maeneo hatarishi ambayo mazingira yake yanaweza kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa hasa wakati wa mvua.

Aidha makamu wa pili wa rais amesema katika kupambana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya mafunzo yataendelea kutolewa kwa wadau katika shehia zenye bandari rasmi na zisizo rasmi.

Zaidi ya shilingi bilioni 44 na milioni mia nane na 37 zimeombwa kuidhinishwa kwa , ofisi ya makamu wa pili wa rais wa zanzibar na taasisi zake kwa ajili ya kutekeleza programu  zake  kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.