SUALA LA TABIA NCHI LINAENDELEA KUKUMBWA NA UTATA

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi amesema suala la tabia nchi linaendelea kukumbwa na utata kutokana na baadhi ya wanadamu kudharau utunzaji wa mazingira kunakopelekea kuzuka kwa migogoro isiyokwisha duniani.

Amesema yapo mataifa mengi duniani hasa  yanayoendelea yaliyoathirika na tabia nchi licha ya

Kuwa dunia ina mazingira mazuri lakini baadhi ya watu wamekuwa wakiyachafua mazingira hayo kwa makusudi.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira na wale wa Idara ya Mazingira  baada ya kutembelea Taasisi hizo hapo Maruhubi ambazo kwa sasa zimehamishiwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Alisema mienendo ya Miongo ya hali ya Hewa hivi sasa imepanguka sambamba na mipangilio ya Kilimo kubadilika kufuatia Wanaadamu kukosa huruma katika matumizi ya mali zisizorejesheka na hatimae uchafuzi wa mazingira umeongezeka kwa asilimia kubwa .

Balozi Seif alifahamisha kwamba zipo Nchi zinazoendelea na Maisha ya kawaida kwa kupata baraka ya mvua kutokana na kuheshimu mazingira yao akitolea mfano Taifa ya Jamuhuri ya Cuba.

Aliwakumbusha Watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira pamoja na Idara ya Mazingira kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kusimamia utunzaji wa Mazingira ili Jamii iweze kustawika vyema.

Akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar baada ya kutembelea Kituo cha Operesheni na Mawasiliano cha Maafa kiliopo Maruhubi Balozi Seif alisema Taasisi hiyo inasimamia jukumu lisiloonekana jambo ambalo watendaji wake wanapaswa kuwa tayari wakati na saa ye yote pale inapotokezea janga la ghafla.

Alisema Jamii ni vyema ikajenga Utamaduni wa kuwa na Imani kwa Watendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa  wakati wanapokumbwa na Maafa katika maeneo yao wanayoishi.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imelazimika kuimarisha zaidi Kitengo cha kukabiliana na Maafa baada ya kupata funzo kubwa lililotokana na maafa ya ajali mbili za Meli ile ya Spice Islan na M.V  Skajit miaka michache iliyopita na kuleta simanzi kubwa miongoni mwa Jamii na Taifa kwa ujumla.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar Nd. Haji Mjaja Haji alisema Taasisi hiyo hupokea Ripoti za Tathmini mbali mbali zipatazo 50 kwa Mwaka ainazohusiana na shughuli za Kimazingira.

Nd. Mjaja alisema Ripoti hizo pia zimefuatiliwa na zile zinazohusiana na masuala ya Mafuta na Gesi Asilia ambazo Taifa linalazimika kuwa makini katika kujiepusha mapema na athari kabla ya kusubiri matokeo mabaya hapo baadae.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukambiliana na Maafa Zanzibar  Nd. Makame Khatib Makame alisema Sekriterieti ya Kukabiliana na Maafa imekuwa ikifanya ukaguzi na Mipango ya Kukabiliana na Maafa ili kuepuka athari mapema.

Nd. Makame alisema vipo vyombo kadhaa vya Usafiri wa Baharini vilivyofanyiwa ukaguzi huo vikiwemo vituo vya Mafuta na kuridhika na Mazingira yaliyomo kwenye vyombo hivyo.

Alisema Ukaguzi huo umeenda sambamba na Daftari Maalum lililowekwa kuratibu Watu wanaokabiliwa na Maafa Kila Mwaka  ambapo Takwimu zinaonyesha uwepo wa Watu 51 waliofikia kigezo cha kuingia katika Daftari hilo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Taasisi hizo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdulla Hassan  Mitawi alisema Wizara hiyo imeziona changamoto zinazozikabili Taasisi hizo mbili na itafanya jitihada katika kuzitafutia ufumbuzi wakudumu.

Nd. Abdulla alisema Taasisi zinayosimamia Masuala ya Kimazingira zinastahiki kupewa kipaumbele kutokana na changamoto kubwa inayowakabili ya ufinyu wa Ofisi kwa Watendaji wao huku ikieleweka kubeba jukumu zito la Taifa la usimamizi wa Mazingira.