TAASISI ZA UMMA NA BINAFSI KUFUATA MFUMO WA MATUMIZI YA FEDHA

 

Taasisi za fedha nchini zimetakiwa kuendelea kuzisaidia taasisi za umma na binafsi kufuata mfumo wa matumizi ya fedha ili kusaidia maendeleo ya taasisi hizo na taifa kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe; Ayoub Mohammed Mahmoud alitoa wito huo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili yaliyoshirikisha wakuu wa taasisi za Serikali na taasisi za kiraia yaliyoandaliwa na benki ya NMB.

Amesema iwapo taasisi hizo zitajengewa uwezo zitaimarisha mifumo yao ya mapato na matumizi jambo litakalosaidia kukuza mapato yao na kudhibiti matumizi kulingana na mageuzi ya kiuchumi kupitia mifumo ya kifedha.

Amesema serikali kupitia mkakati wa kukukuza uchumi na kupunguza umaskini Zanzibar (mkuza) imefanya mabadiliko kadhaa katika sekta ya fedha yaliyolenga kukuza mapato ya Serikali, mashirika ya umma na taasisi zisizo za kiraia hivyo taasisi hizo zinapaswa kuhakikisha zinatumia huduma za kibenki zinazotolewa na benki hiyo ili kujiendeleza.

Nao washiriki wa mafunzo hayo walisema kuwa yamewasiadia kujua huduma mbali mbali za kifedha zinazotolewa na benki hiyo sambamba na kuwajengea uwezo ambao watautumia katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kudhibiti matumizi yao kwa manufaa ya wanachama wa taasisi hizo na jamii kwa ujumla.

Akitoa maelezo kuhusu mafunzo hayo mkuu wa biashara za kitaasisi kutoka makao makuu ya benki ya NMB William makoresho amesema mafunzo hayo yalilenga kuonesha shughuli zinazofanywa na benki yake kwa baadhi ya wateja wake ili waweze kuzitumia kwa lengo la kuimarisha utendaji wa taaisisi hizo.

Amesema watu wengi wanafikiria benki yake inafanya kazi ya kutunza fedha au kutoa mikopo kwa wateja wake tu bali kupitia semina wameweza kujua mahitaji ya wateja wao na kuwataka kuendelea kutumia huduma za benki hiyo kikamilifu.

Nae meneja wa benki hiyo tawi la Zanzibar Abdallah Duchi amesema katika siku mbili za mafunzo hayo benki hiyo imeweza kuwafikia Wakurugenzi wa taasisi na mashirika ya serikali, Wakurugenzi wa taasisi za kiraia na Wakuu wa taasisi za elimu ya juu ili kuwajengea uwezo juu ya namna bora ya kuongeza mapato na tija ya taasisi zao.