TIMU YA SOKA YA HOTELI YA SEA CLIFF IMETWAA UBINGWA

 

 

Timu ya soka ya hoteli ya sea cliff  imetwaa ubingwa wa kombe la Mwakilishi na Mbunge wa Jimbo la Mahonda baada ya kuitandika Timu ya Soka ya  King Power ya Fujoni kwa Goli 2-1 katika mchezo wa Fainal uliochezwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Misuka uliopo Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Pambano hilo kali na la kusisimuwa la Fainali limewafanya wapenzi na watazamaji wa Soka kushindwa kukaa chini kwa dakika zote za Mchezo kutokana na umahiri wa wachezaji walioufanya mchezo huo kuwa wa kuvutia na uliojaa nguvu za ziada kwa wachezaji wa Timu zote mbili.

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi na Mbunge wa Jimbo hilo Bahati Abeid  Nassir walikuwa miongoni mwa Wadau wa Soka walioshuhudia pambano hilo la Fainali ya aina yake lililonasa pia wapita njia waliolazimika kukwama na kushuhudia mtanange huo uliofanyika uwanja wa Misuka Mahonda.

Wababe wa Sea Cliff  waliovalia jezi rangi ya Manjano ndio walioanza kuziona nyavu za wapinzani wao King Power kwa kuandika Goli la kwanza Sekunde 24 tu tokea kuanza kwa pambano hilo lililofungwa na mchezaji machachari Muhammad Said ambae kwa umahiri wake akapachika tena Goli la Pili katika Dakika ya Kwanza na Sekunde 50 ya Mchezo kwenye Kipindi hicho cha Kwanza.

Said Ali wa Timu ya Soka ya King Power akaiandikia Goli Timu yake katika Dakika ya 6 ya Mchezo kipindi hicho cha Kwanza na kupelekea wakienda mapumziko matokeo yakabakia kuwa Sea Cliff  ikiongoza kwa Goli 2 dhidi ya King Power waliotoka na Goli 1.

Kipindi cha Pili kilichoanza kwa kasi ile ile ya mchezo huo wa Fainal kiliwafanya wachezaji wa Kingi Power kusaka Goli la kusawazisha kwa kupelekea mashambulizi ya mfululizo, lakini ngome ya Sea Cliff ilijaribu kudhibiti mashambulizi hayo.

Hadi mwisho wa Fainali hiyo Sea Cliff walitoka na ushindi wa Bao 2-1 dhidi ya King Power licha ya vijana hao wa Fujoni kumlalamikia Mwamuzi wa Mchezo huo kuwabeba zaidi wachezaji wa Timu ya Sea Cliff na kulazimika Viongozi wa Timu hiyo kutumia busara na hekima kuhakikisha Timu yao inakamilisha utararibu wote wa kumalizika kwa Mchezo huo wa Finali.

Akikabidhi Kikombe kwa Mabingwa hao wa  Hoteli ya Sea Cliff pamoja na zawadi ya Fedha Taslim, Seti za Jezi pamoja na Mipira kwa Timu zilizofanya vyema kwenye Mashindano hayo, Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi wanamichezo pamoja na wapenzi wao kujiepusha na michezo isiyostahiki wakati wakiwa Uwanjani.

Balozi Seif alisema kinachopaswa kuzingatiwa zaidi na wanamichezo viwanjani ni kudumisha nidhamu itakayowawezesha wapenzi kuridhika na kinachotendeka kwenye maeneo hayo ya michezo badala ya vurugu na vitendo visivyostahiki.

Balozi Seif alisema katika kuunga mkono jitihada za Viongozi na wanamichezo hao wa Soka wa kuendeleza mchezo huo aliahidi kwamba Uongozi wa Jimbo la Mahonda utayaendeleza Mashindano hayo kila mwaka  ili kutoa fursa kwa kila Kijana mwenye kipaji kutumia nafasi hiyo kujitangaza vyema mbele ya macho ya Wanasoka Nchini.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mahonda  Bahati Abeid Nassir  alisema Mashindano ya Kombe la Mwakilishi na Mbunge wa Jimbo la Mahonda yameonyesha kiwango kinachorodhisha katika soka ndani ya Jimbo na kuleta furaha kwa Wapenzi wa mchezo huo.

Bahati alisema Viongozi wameamua kuandaa mashindao hayo katika kuwakuitanisha wachezaji wa Timu tofauti lengo likiwa kujaribu kutafuta mbinu na maarifa ya kuibua Vipaji vya Vijana kwa vile Mpira hivi sasa ni ajira ya kudumu inayostawisha maisha bora ya Vijana wanaojishugfhulisha na mchezo huo.

Katika Fainali hiyo ya Kombe la Mwakilishi na Mbunge wa Jimbo la Mahonda Viongozi hao walikabidhi Fedha Taslim kwa Timu zilizofanya vyema kwenye ngazi ya Wadi mbili za Mahonda na Fujoni, kutoa Seti za Jezi pamoja na Mipira vyote vikiwa na Thamani ya Shilingi za Kitanzania Milioni 5,300,000/-