TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA KUDHIBITI DAWA ZA KULEVYA

 

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema hatma ya zanzibar kuhusu dawa za kulevya imo mikononi mwa tume ya kitaifa ya kuratibu na kudhibiti dawa hizo iliyoundwa kusimamia kukabiliana nazo.

Ameeleza kuwa wakati wajumbe wa tume hiyo wakijipanga na mapambano hayo lazima wafahamu kuwa ni vita vikali vinavyohusisha watu wenye fedha nyingi na mtandao mkubwa.

Akiizindua rasmi tume hiyo ya kitaifa ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya hapo ofisini kwake vuga mjini zanzibar akiwa yeye ndie mwenyekiti wa tume hiyo  balozi seif ali iddi alisema mafanikio ya tume hiyo yatategemea zaidi jindi wajumbe wake watakavyojipanga vizuri kwa kushirikiana  kwa karibu zaidi na wadau wengine katika kukabiliana na uingizwaji wa dawa hizo nchini.

Balozi seif alisema hali ya utumiaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini kote sio mzuri hali iliyopelekea serikali zote mbili kulivalia njuga tatizo hilo sugu la dawa za kulevya lenye kuiangamiza jamii hasa vijana ambao ndio nguvu kazi kubwa ya taifa.

Alisema kwa kuwa wanaojishughulisha na dawa za kulevya baadhi yao wanaeleweka na wanaishi pamoja na jamii mitaani. Hivyo ni vyema jukumu la wajumbe wa tume hiyo likaelekeza zaidi nguvu zake katika uzuiaji wa uingizaji wa dawa hizo hapa nchini sambamba na kutoogopa kuwachukulia hatua za kisheria wahusika hao.

Balozi seif alisisitiza kwamba kwa kuwa suala la dawa za kulevya linazikumba pembe zote za dunia, mafanikio ya vita hivyo yatahitaji mashirikiano ya taasisi za ndani na nje ya nchi ambazo zinajihusisha moja kwa moja na dawa hizo thakili.

Makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi seif alimshukuru rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi zanzibar dr. Ali mohamed shein mwa imani aliyokuwa nayo kwake  kwa kumteua kuwa mwenyekiti wa tume hiyo.

Aidha balozi seif aliwapongeza wajumbe wote walioteuliwa kushirikiana naye katika utekelezaji wa jukumu hilo zito ambalo anaimani kwamba kila mjumbe analiweza licha ya uzito uliopo mbele yao.

Balozi seif  aliwakumbusha wajumbe wa tume hiyo  wajibu wao kwa mujibu wa kifungu cha 4 {1} cha sheria  wa kusimamia mambo tisa akiyataja baadhi yake kuwa ni pamoja na kuandaa na kusimamia utekelezaji wa mpango wa taifa za udhibiti wa dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa sheria nambari 9 ya mwaka 2009  kifungu cha 4 {1} tume ya kitaifa ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya  wajumbe wake wana wajibu wa kukutana mara mbili kwa mwaka.