UBORESHAJI WA HUDUMA ZA AFYA KWA WANAWAKE NCHINI ZIMEENDELEA KUZAA MATUNDA

Jitihada za Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kusaidia uboreshaji wa huduma za afya kwa wanawake nchini zimeendelea kuzaa matunda baada ya Taasisi ya Merck yenye makao yake makuu nchini Ujerumani kumwahidi kuaanzisha mpango wa kugharamia Mafunzo maalum kwa wataalamu wa afya nchini hususan kwenye maeneo ya Saratani kwa watoto, matibabu ya saratani kwa upasuaji na utabibu kwa tanzania bara na Zanzibar.

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Merck Dkt Rasha kelej ametoa kauli hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ikulu jijini dar es salaam na kusema kuwa taasisi hiyo imejitolea kuisaidia Serikali ya Tanzania katika jitihada zake za kuboresha sekta ya afya kwa Tanzania Bara na Zanzibar kupitia mpango huo unaotarajiwa kuanzishwa mwishoni mwa mwaka huu.

Dkt Rasha Kelej amesema mafunzo hayo kwa wataalamu wa afya yatatolewa kwa muda wa mwaka mmoja hadi mitatu katika mataifa ya India, Ulaya na Kenya lengo likiwa ni kuboresha upatikanaji wa huduma zote zinahusu saratani hapa nchini.

taasisi ya Merck pia imemhakikishia makamu wa Rais kuwa watajikita katika kuwajengea uwezo akina mama wenye matatizo ya ugumba kwa kuhakikisha wanapata taarifa sahihi zinazohusia na matatizo ya ugumba hivyo itasaidia kubadilisha mtazamo ambao umejengeka kwenye jamii kuhusu masuala ya ugumba kwa akina mama.

ajenda hii itasimamiwa kupitia programu ya Merck more than a mother.                                                                   

aidha, makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ameipongeza taasisi ya merck kwa juhudi zao za kuboresha sekta ya afya Barani Africa na amewakaribisha kufanya kazi nchini Tanzania.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema amefurahishwa na mipango na mikakati ya taasisi hiyo na kwamba Serikali iko tayari kushirikiana na Merck Foundation katika kuwajengea uwezo kina mama pamoja na utoaji wa mafunzo kwa wataalamu mbalimbali  wa sekta ya afya nchini hasa kwenye matatizo yaSaratani na ugumba kwa ujumla.

 

kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa watendaji wa taasisi hiyo zinaonyesha kuwa tatizo la ugumba kwa wanandoa barani Africa ni kubwa ambapo inakadiriwa kwamba katika kila ndoa nne, moja inasumbuliwa na changamoto ya ugumba na karibu asilimia 85 ya ugumba inasababishwa na ukosefu wa matibabu kwa magonjwa ambayo yanaweza kutibika.