UHAMIAJI YAPONGEZWA KWA MAFANIKIO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Idara ya Uhamiaji Tanzania kwa kuendelea kupata mafanikio na kusisitiza haja ya mafunzo kwa wafanyakazi wa Idara hiyo ili iendelee kufanya kazi kwa ufanisi zaidi hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Kamishna Jenerali mpya wa Uhamiaji Tanzania Dk. Anna Peter Makakala, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha rasmi kwa Rais.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alimueleza Kamishna Jenerali Makakala kuwa Idara ya Uhamiaji Tanzania ni Idara kongwe ambayo imeweza kupata mafanikio makubwa kutokana na uzoefu mkubwa uliopo kwenye Idara hiyo, hivyo suala la mafunzo linahitajika ili Idara hiyo iendelee kufanya kazi kwa wakati uliopo.
Aidha, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa licha ya mafanikio yaliopo pia zipo changamoto ambazo kwa mashirikiano ya pamoja zinaweza kutatuliwa huku akipongeza juhudi za Idara hiyo za kujenga Ofisi mpya za Makao yake makuu kwa upande wa Zanzibar.
Dk. Shein aliongeza kuwa ipo haja kwa Idara hiyo kuwandaa wafanyakazi wake kwa kuwapatia mafunzo yanayoendana na kazi zao kwani kazi hiyo inahitaji mafunzo na utaalamu unaoenda sambamba na kazi hiyo hasa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia duniani ambapo Idara hiyo inapaswa kwenda sambamba na hali hiyo.
Alisisitiza umuhimu wa kuwasikiliza na kuwawezesha wafanyakazi ili waendelee kuwa na ari ya kufanya kazi zao kwa ustadi na kuweza kupata mafanikio zaidi ha ikizingatiwa kuwa sayansi na teknolojia imezidi kukua duniani.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Mkuu huyo wa Uhamiaji kuwa kuna umuhimu wa kuendeleza mashirikiano na vikosi vyengine vya ulinzi na usalama hapa nchini ili Idara hiyo iweze kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliendelea kutoa pongezi kwa Idara hiyo kwa kuendelea kufanya kazi vizuri na kwa mashirikiano kati ya wafanyakazi na viongozi wakuu wa Idara hiyo waliopo Zanzibar na wale waliopo Tanzania Bara.
Nae Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Tanzania Dk. Anna Peter Makakala alitoa shukrani kwa Dk. Shein kwa kuendelea kuiunga mkono Idara hiyo na kumueleza kuwa licha ya kazi zake inazofanya Idara hiyo ya Uhamiaji pia, ina kazi ya kukusanya mapato.

Kamishna Makakala alieleza kuwa azma ya Idara hiyo ni kuelekea kwenye teknolojia zaidi na juhudi za makusudi zimekuwa zikiendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Alieleza kuwa licha ya baadhi ya changamoto zilizopo katika Idara hiyo ambazo zinaendelea kupatiwa ufumbuzi suala la mafunzo kwa wafanyakazi wake limepewa kipaumbele kwa kiasi kikubwa.
Aliongeza kuwa Idara ya Uhamiaji ni Idara ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo itaendelea kufanya kazi zake kwa mashirikiano ya pamoja katika maeneo yote ya ndani ya Jamhuri hiyo ya Muungano wa Tanzania yaliopo Tanzania Bara na Zanzibar.
Pia, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji huyo, alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Idara hiyo itaendelea kufanya kazi kwa mashirikiano na vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama nchini Tanzania kwa kutambua umuhimu huo katika kufikia lengo walilojiwekea katika utendaji wao wa kazi.