UHUSIANO WA KARIBU BAINA YA OMAN NA ZANZIBAR UNAZIDI KUKUA.

Uhusiano wa karibu baina ya Wizara ya Habari, Utalii na mambo ya Kale Zanzibar na mamlaka ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa ya Oman unaendelea kukua kila wakati kufuatia ukaribu uliopo wa viongozi wa kitaifa wa Oman na Zanzibar.

Mwenyekiti wa mamlaka ya Nyaraka na Makumbusho ya Kitaifa wa Oman Dr. Hamad Mohamed  Al – dhawyany ametoa kauli hiyo akiuongoza ujumbe wa viongozi 12 wa taasisi hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu waPili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi vuga Mjini Zanzibar.

Dr. Hamad Mohamed  Al – dhawyany alisema Historia ya kidamu muda mrefu iliyopo kati ya wananchi wa Zanzibar na Oman inazidi kuongeza ushawishi wa ushirikiano katikanyanja tofauti zinazozidi kuongezeka siku hadi siku.

Alisema uimarishaji wa jumba la ajabu Forodhani, pamoja na magofu ya kihistoria yaliyopo Mtoni chini ya ufadhili wa Oman utakapokamilika utatoa fursa kwa wageni na watalii kutembelea kitendo ambacho mbali ya kuimarisha historia hiyo muhimu lakini pia kitaongeza mapato ya taifa.

Dr. Hamad Mohamed  Al – dhawyany alisema wakati matengenezo ya Jumba la Ajabu Forodhani yakiendelea pamoja, magofu ya kihistoria yaliyopo mtoni ujenzi wake unaweza kuanza wakati wowote kuanzia sasa kwa vite taratibu zote zimeshakamilika.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar inathamini sana ushirikiano wake na Oman kutokana na Historia ya wananchi wake walioingiliana kidamu.

Balozi Seif aliendelea kuipongeza Serikali ya Oman chini ya kiongozi wake Mahiri Mfalme Qaboos Bin Said kwa jitihada inazochukuwa za kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kujiletea maendeleo yaliyolenga kustawisha maisha ya wananchi wake.

Alisema ujio wa meli ya kifalme ya Oman katika visiwa vya Zanzibar miaka miwili iliyopita mbali ya wananchi wa Zanzibar  kufurahia ujio huo lakini pia imeleta baraka kubwa kutokana na mambo makubwa yaliyozaliwa kutokana na ziara ya meli hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba matengenezo ya jumba la ajabu forodhani, pamoja na magofu ya kihistoria ya mtoni ni miongoni mwa mambo yaliyozaliwa kutokana na ziara ya meli hiyo.

Balozi Seif alieleza kwamba majengo hayo yana heshima kubwa duniani kutokana na historia yake inayothaminiwa pia na shirika la umoja wa mataifa la elimu, sayansi na utamaduni {unesco}  na kupelekea mji mkongwe za Zanzibar uliobeba majengo hayo kuingizwa katika urithi wa kimataifa.

Mapema waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo alisema hii ni mara ya pili kwa ujumbe wa mamlaka hiyo kutembelea Zanzibar kufuatilia maendeleo ya mikataba mbali mbali iliyotiwa saini kati ya Serikali za Oman na Zanzibar.

Mh. Mahmoud alisema yapo mafanikio makubwa ya utekelezaji wa miradi ya pamoja ya pande hizo mbili akitaja kuwa ni pamoja na matangenezo ya beit al ajaib Forodhani, pamoja na majengo ya kihistoria ya Mtoni.

Comments are closed.

Powered by Live Score & Live Score App