UMUHIMU WA KUYATUNZA MAZINGIRA KWA FAIDA YA VIUMBE MBALIMBALI

Katika kuelekea maadhimisho ya siku ya mazingira duniani idara ya mazingira imeamua kuwashirikisha wadau mbali mbali katika uhifadhi wa uoto wa asili ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Katika hatua hiyo idara hiyo imeanza kuvishirikikisha vyuo vya qur-an kutembelea maeneo ya hifadhi ya asili na kufahamu mapema suala la kuhifadhi mazingira ili lizungumzwe katika mafunzo yao.
Wanafunzi kutoka madrasa mbili za zanzibar wametembelea eneo la hifadhi ya jozani na ghuba ya chwaka ili kuona umuhimu uliopo wa kuyatunza mazingira kwa faida ya viumbe mbalimbali pamoja na kujilinda dhidi ya athari za kimazingira ambapo wameelezea suala hilo linawapa uhalisia jinsi mazingira yanavyohifadhiwa baada ya kujifunza nadharia wakiwa skuli.
Akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi hao mtembezaji wageni katika hifadhi ya jozani na ghuba ya chwaka amesema kwa kiasi kumekuwa na mwamko kwa jamii katika kusaidia suala la uhifadhi wa mazingira.
Kaimu mkurugenzi idara ya mazingira alawi haji hija amesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kutokuwa na mipaka ni jukumu kwa jamii kuliangalia kwa upana suala la uhifadhi wa mazingira ikiwemo kushirikiana na taasisi zilizopo katika kubaini maeneo yaliyoathirika ili kuondosha athari hizo.