USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI KATIKA MIRADI UTADUMU UENDESHAJI WAKE.

 

Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya kiuchumi inayowekezwa kwenye maeneo yao itasababisha kudumu kwa muda mrefu katika uendeshaji wake.

Amesema kinyume na utaratibu huo ambao unastahiki kuendelea kusimamiwa na taasisi zinazotoa vibali, inaweza kuzusha migogoro baina ya wananchi na wawekezaji.

Balozi seif ali iddi alitoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara fupi ya kuangalia eneo linalotarajiwa kutaka kuanzishwa kwa ujenzi wa mradi wa kituo cha upigaji mbizi {diving} katika mwambao wa matembwe unaosimamiwa na uongozi wa hoteli ya sun rise.

Alisema ipo baadhi ya miradi ya uwekezaji inayopata baraka zote za serikali katika uanzishwaji wake kupitia taasisi husika lakini kinachojichomoza baadae ni kufifia kwa miradi hiyo kunakotokana na ujanja wa baadhi ya watu kutia mikono yao kwa kutaka kuendeleza ubinafsi.

Balozi seif alisema tabia hiyo kamwe haitoendelea kuvumiliwa na serikali kuu kwani lengo la kuweka milango wazi ya kuanzishwa kwa miradi ya kiuchumi ni kuwapa fursa za kupata ajira wananchi wake ili kuongeza kipato chao na kupunguza umaskini.

Makamu wa pili wa rais wa zanzibar aliuagiza uongozi wa hoteli ya sun rise kusubiri maamuzi ya serikali kuu kuhusu uanzishwaji wa mradi wao wa kituo cha upigaji  mbizi matemwe ili kutafakari mawazo ya baadhi ya taasisi.

Alisema serikali ya mapinduzi ya zanzibar isingependa kuona mradi huo muhimu kwa kuchochea sekta ya utalii zanzibar unakumbwa na changamoto zinazoweza kuepukwa mapema likiwemo suala la kimazingira.

Mapema mkurugenzi uwezeshaji na miradi ya maendeleo wa mamlaka ya uwekezaji vitega uchumi zanzibar {zipa} nd. Sharif  ali sharif  alisema taasisi ya uwekezaji hufikia maamuzi ya kutoa ruhusa ya kuanzishwa kwa mradi wa uwekezaji baada ya mmiliki wa mradi husika kukamilisha taratibu zote zinazomruhusu kuwekeza nchini.

Nd. Sharifu alimueleza makamu wa pili wa rais wa zanzibar kwamba miongoni mwa taratibu hizo ni ushirikishwaji wa wataalamu wa taasisi zote zilizopewa jukumu la kusimamia masuala ya miradi na uwekezaji wakiwemo sambamba na wawakilishi wa wananchi katika maeneo husika.

Akiwasilisha salamu za wananchi wa ukanda wa mwambao wa matemwe, diwani wa wadi ya mwatemwe ndugu hassan mcha hassan alisema mradi wa hoteli ya sun rise umeleta mafanikio makubwa kwa wananchi wake tokea ulipoanzishwa  kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

Nd. Hassan alisema wananchi wa matemwe wamelazimika kumuenga enga muwekezaji huyo kutokana na juhudi kubwa anazoendelea kuzichukuwa za kuwasogezesha miundombinu katika kuwarahisisha mambo yao ya maendeleo ya kila siku.

Alisema kitendo cha uongozi wa sun rise cha kupeleka huduma za umeme kijijini hapo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni  mia 128,000,000/-  kimewawezesha wananchi hao  pamoja na wanafunzi wa skuli za vijiji hivyo kupata huduma za umeme zilizorahisisha pia upatikanaji wa huduma za maji safi na salama