UTURUKI IMEDHAMIRIA KUENDELEA NA OPERESHENI YAKE

 

Rais wa uturuki recep tayyip erdogan amesema kuwa uturuki imedhamiria kuendelea na operesheni yake kali dhidi ya wapiganaji wa kikurdi nchini syria.

Erdogan ameyasema hayo wakati wanajeshi wa uturuki wakikabiliwa na upinzani mkali katika siku ya tatu ya uvamizi wake katika mji wa afrin.

Uturuki ilianzisha mashambulizi ya nchi kavu ili kuwafurusha wapiganaji wa kikurdi kutoka kwenye mipaka yake ya kusini na kuzuia kuundwa kwa jimbo dogo linalotawaliwa na wakurdi ambalo huenda likayadhoofisha zaidi maeneo yenye wakurdi wengi nchini uturuki.

Wakurdi wa syria wameanzisha mashambulizi makali jumapili jioni, na kuwaondoa wanajeshi wa uturuki na washirika wao kutoka kwenye vijiji viwili walivyokuwa wamevikamata kwa muda mfupi.

Karibu wapiganaji 26 wa kikurdi na waasi 19 wanaoiunga mkono uturuki wameuawa katika siku tatu za mapigano na pia raia wengine 24 waliripotiwa kuuawa katika mapambano hayo.