UWEZEKANO WA KUWAPOTEZA VIUMBE KASA WASIPOHIFADHIWA

 

Naibu waziri wa kilimo,maliasili,mifugo na uvuvi mh. Lulu msham khamis ameeleza kuwa juhudi za kuwahifadhi kasa zisipozingatiwa upo uwezekano wa kuwapoteza viumbe hao ambao ni moja ya kivutio katika ya sekta ya utalii na ni sehemu ya kutoa ajira kwa vijana.

Akishiriki katika zoezi la kuwaachilia kasa baharini ambalo hufanyika kila mwaka katika kijiji cha nungwi mnarani mh.lulu amesema imebainika kuwa sababu zinazochangia kutoweka kwa viumbe hao ni kutozingatiwa kwa utunzaji wa mazingira katika fukwe na kunasa katika mitego ya wavuvi.

Hivyo amewataka wananchi kuendelea kuwahifadhi kasa na serikali itaendelea kuwapa ushirikiano ikiwemo kuwapatia mafunzo wanajumuiya wanaojishughulisha na ufugaji wa kasa.

Akisoma risala ya jumuiya nd. Ali ibrahim ameelezea tatizo la muda mrefu linalowakabili ikiwemo kuwepo kwa tope katika bwawa la kufugia viumbe hao, ambapo nd .ali pondo hamad ameelezea namna mradi unavyowanufaisha.

Wakaazi wa kijiji cha nungwi walioshuhudia tukio la kuachiliwa kasa 85 kuelekea baharini  wamesema mradi huo umewasaidia katika utunzaji wa mazingira na kuwawezesha kujikimu kimaisha.