VIJANA WENGI ZAIDI WANAHITAJI KUSOMESHWA NA KUSAIDIA KUKOPESHWA WAPATE KUJIENDELEZA.

Rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk. Ali mohamed shein, ameitaka bodi ya mikopo elimu ya juu zanzibar kutoa mikopo kwa wakati na kuangalia namna ya kuwakopesha wanafunzi fedha za kujikimu.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, alipokutana na uongozi wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali, bodi ya wakurugenzi ya bodi ya mikopo elimu ya juu pamoja na uongozi wa bodi hiyo katika vikao vinavyoendelea ikulu mjini zanzibar.

Dk. Shein alieleza matumaini yake juu ya bodi hiyo kuwa itaendelea kupata mafanikio makubwa zaidi na kusisitiza kuwa vijana wengi zaidi wataendelea kusomeshwa na kusaidia kukopeshwa wapate kujiendeleza.

Pamoja na hayo, dk. Shein alieleza haja ya kutafutiwa utaratibu maalum kwa wale wote waliokuwa bado hawajaanza kurejesha fedha ambao hata kupatikana kwao kuna ugumu na kutoa muda maalum wa kufanyiwa kazi suala hilo.

Aidha, aliipongeza bodi, wizara, uongozi kwa mafanikio yaliofikiwa na kueleza matumaini yake ya kuzidi kupata mafanikio huku akieleza haja ya kuwaandaa wanafunzi katika vyuo na skuli kwa ajili ya masomo maalum.

Nae waziri wa elimu na mafunzo ya amali riziki pembe juma aliupongeza mfuko wa zssf kwa kuanza kutoa mikopo kwa wafanyakazi wanaojiendeleza kielemu badala ya kutegemea mkopo kutoka bodi hiyo ambapo pia, wafanyakazi wa sekta binafsi nao watafaidika.

Mwenyekiti wa bodi kombo hassan juma alisema kuwa mwishoni mwa mwaka 2012 kwa mara ya kwanza bodi ilianzisha utaratibu wa kurejesha mikopo kama sheria inavyoagiza na makusanyo yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka  ambapo hivi sasa tayari imeweza kukusanya zaidi ya tzs milioni 100 kwa mwezi na kwa mwaka 2017/2018 wanakusudia kukusanya marejeshi ya tzs 1.5 bilioni.

Alieleza kuwa bodi imejitahidi kuwa na mahusiano ya karibu na bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ya serikali ya muungano hususan katika kubadilisha taarifa za wanafunzi wanaopatiwa mikopo na mafunzo ya vitendo kwa wafanyakazi.

Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa kuwepo na kuimarika kwa taasisi hiyo kutachangia maendeleo ya taifa kwa kuongeza wataalamu wazalendo katika fani za aina mbali mbali.

 

Nao uongozi wa bodi ya mikopo zanzibar ulieleza kuwa katika kipindi hiki cha miaka sita tokea kuanzishwa kwake, bodi ya mikopo ya elimu ya juu imetoa mikopo kwa wanafunzi wapya 5,100 na wanafunzi 881 iliyowarithi kutoka uliokuwa mfuko wa elimu ya juu.

Ulieleza kuwa fedha ambayo ipo mikononi mwa wahitimu wa kuanzia mwaka wa masomo 2006/2007 hadi mwaka 2015/2016 na inayopaswa kuanza kurejeshwa ni tzs 33.2 bilioni zikijumuisha tzs 7.8 bilioni zikiwa ni deni lililorithiwa  kutoka kwa wadaiwa waliokopeshwa na uliokuwa mfuko wa elimu ya juu.

 

Uongozi huo ulieleza kuwa umekuwa ukichukua hatua mbali mbali kuwatafuta wadaiwa 2,899 ambao hawajaanza kurejesha mikopo ili waweze kufanya taratibu za kurejesha mikopo hiyo.

Akieleza miongoni mwa mafanikio yaliopatikana, mkurugenzi huyo alieleza kuwa ni pamoja na kuongeza kasi ya marejesho ambapo wahitimu wengi wameanza kujitokeza kuhakiki madeni yao na kuanza kurejesha mikopo yao.

 

Wakati huo huo, dk. Shein alikutana na bodi ya baraza la elimu ambapo alieleza kuwa uzalendo, uwajibikaji, usimamizi na uongozi katika sekta hiyo hasa katika skuli ni suala muhimu na lalazima kwa lengo la kuimarisha sekta ya elimu.

Waziri wa elimu na mafunzo ya amali, riziki pembe juma alieleza kuwa uhakikiki wa walimu umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa pamoja na kusimamia ada kwa skuli binafsi na kueleza kuwa chombo hicho pia, kimekuwa kikisimamia kesi za udhalilishaji licha ya kuwepo baadhi ya changamoto katika kupatikana muwafaka wake.

Aidha, alieleza azma ya wizara yake katika kuvisajili vituo vinavyotoa elimu ya ziada na kueleza juhudi zinazoendelea katika usajili wa skuli za binafsi na  serikali.

Katibu mkuu kiongozi na katibu wa baraza la mapinduzi dk. Abdulhamid yahya mzee alieleza haja ya kuwepo utaratibu maalum katika kuangalia faida na athari za masomo ya ziada kwa wanafunzi hasa kutokana na utamaduni huo kuzidi kuimarika hivi sasa.

Mwenyekiti wa bodi ya baraza hilo la elimu bi saad thani fakih aliyaeleza miongoni mwa mafanikio yaliopatikana ikiwa ni pamoja na kuzipatia usajili wa kudumu baadhi ya skuli za binafisi, kufanya ziara ya kuzitembelea skuli binafisi na za serikali pamoja na kupitisha ada mpya ya malipo ya skuli za binafsi na leseni za walimu.

Nae mrajis wa elimu na katibu wa baraza la elimu zanzibar siajabu suleiman pandu alieleza mafanikio na changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa usajili wa skuli za kimataifa na uanzishwaji wa vyuo vya ualimu huku akieleza kuwa tayari skuli 452 za serikali na 390 za binafisi zimepatiwa usajili.

Rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk. Ali mohamed shein alimaliza vikao vyake vya leo kwa kukutana na bodi ya baraza la mitihani zanzibar ambapo katika maelezo yake alitoa pongezi na kulitaka baraza la mitihani zanzibar kuongeza kasi katika utendaji wake wa kazi ili liendelee kupata mafanikio zaidi.

Mwenyekiti wa bodi ya baraza la mitihani mariam abdallah yussuf alitoa pongezi kwa serikali ya mapinduzi ya zanzibar kwa kuliwezesha baraza hilo kuendesha mitihani ya taifa inayosimamiwa na baraza hilo ambayo ni mitihani ya elimu ya msingi na ile ya kumaliza elimu ya sekondari ya awali (kidato cha pili) na ualimu.

Alieleza kuwa baraza hilo ni mwanachama wa umoja wa mabaraza ya mitihani afrika (aeaa) na hushiriki katika vikao vyake ili kupata uzoefu wa namna ya uendeshaji wa shughuli za mabaraza ya mitihani katika nchi mbali mbali.

Mkurugenzi wa baraza hilo, zubeir juma khatib kwa upande wake alieleza kuwa dhamira ya baraza hilo ni kutoa tathmini thabiti na inayoaminika kwa mitihani ya elimu ya msingi, sekondari ya awali na ualimu ambayo itaimarisha elimu na kukidhi viwango vya elimu ya taifa na kimataifa.