VIKOSI VYA UTURUKI VIMEPAMBANA NA WAPIGANAJI WA KUNDI LA MUUNGANO HAYAT TAHRIR AL-SHAM

Vikosi vya uturuki vimepambana na wapiganaji wa kundi la muungano linalojiita hayat tahrir al-sham, katika jimbo la idlib lililopo mpakani mwa uturuki na syria, siku moja baada ya uturuki kutangaza kuanzisha operesheni yake katika jimbo hilo.
Uturuki ambayo inawaunga mkono waasi, pamoja na urusi na iran zinazounga mkono serikali ya syria, mapema mwaka huu wamekubaliana juu ya mpango wa kusitisha mapigano katika maeneo manne nchini syria likiwamo jimbo la idlib, kama njia ya kusitisha mapigano na mwanzo wa mazungumzo ya kuleta amani katika nchi iliyoharibiwa na vita.
Kundi hilo linatajwa kudhibiti karibu jimbo lote la idlib. Zaidi ya watu laki tatu wameuawa nchini syria tokea mgogoro huo wa wenyewe kwa wenyewe kuanza baada ya maandamano ya kuipinga serikali mwezi machi 2011.