WAKATI MUAFAKA KWA SKULI ZA ZANZIBAR KUTUMIA MPANGO

 

Makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi seif ali iddi amesema ni wakati muafaka kwa skuli za zanzibar kutumia mpango kazi ambao uongozi wa skuli husika unapaswa ukusanye matokeo baada ya mitihani ili kufanya uchambuzi utakaobainisha maeneo yanayotakiwa kufanyiwa  kazi.

Amesema uongozi wa skuli ukijipanga upya  kwa kushirikisha wanafunzi katika kukabiliana na kasoro zilizozorotesha matokeo ya wanafunzi waliopita inakuwa rahisi kutekeleza waliyokubaliana na kuleta mafanikio.

Balozi seif ali iddi ambae pia ni mwakilishi wa jimbo la mahonda alieleza hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na waziri wa elimu na mafunzo ya amali zanzibar mh. Riziki pembe juma wakati wa hafla maalum ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao ya taifa ya kidato cha pili na cha nne katika skuli ya sekondari ya mahonda.

Alisema utaratibu au mpango kazi huo wa kupata mafanikio endelevu ya elimu   { systematic quality work } ukifuatwa  ipasavyo kila mwaka utasaidia kunyanyua ufundishaji na hatimae skuli za zanzibar  zitanyanyua viwango vya ufaulu.

Alisema ni jukumu la wizara ya elimu na mafunzo ya amali zanzibar kuhakikisha kwamba  skuli zote nchini zinawekewa utaratibu maalum wa kuzipima kila mwisho wa mwaka kwa lengo la kunyanyua ubora wa skuli zote visiwani zanzibar.

Aliwapongeza wanafunzi wote wa skuli ya sekondari ya mahonda waliofaulu vizuri mitihani yao na kusema kwamba mafanikio yaliyopatikana  hayakuja kama mvua bali ni matunda ya mshikamano yaliyoonyeshwa baina ya walimu, wazee kamati ya skuli pamoja na wanafunzi wenyewe.

Aliushukuru uongozi wa skuli ya mahonda pamoja na kamati ya wazazi ya skuli hiyo  kwa uamuzi wake wa busara wa kutenga siku maalum ya kuwapongeza vijana wao waliofaulu vyema katika mitihani yao ya kidato cha pili na cha nne.

Akisoma risala ya walimu, wanafunzi na wazazi wa skuli ya mahonda mwalimu wa sekondari wa skuli hiyo mwalimu dadi salim rashid alisema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi waliofanya mitihani ya kidato cha pili na cha nne kimeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita  nyuma.

Mwalimu dadi alisema idadi ya wanafunzi waliofaulu kwa kidato cha pili imefikia wanafunzin106 kati ya wafafunzin177 waliofanya mitihani wakati kidato cha nne  mwanafunzi pekee wa daraja la pili ndani ya wilaya ya kaskazini b ametokea skuli hiyo ya sekondari mahonda.

Hata hivyo mwalimu dadi alisema skuli ya sekondari  ya mahonda bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazozorotesha ufanisi wa kufanya vizuri wanafunzi wake akizitaja baadhi  yake kuwa ni pamoja na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na kutomalizika kwa ukumbi wao wa mitihani.

Mapema mkuu wa wilaya ya kaskazini “b” nd. Issa  juma ali alisema sababu zinazopelekea wanafunzi kukosa kufaulu mitihani yao ni dhima inayobebwa na wazazi ambao baadhi yao hupenda kuisukumia lawama serikali kuu iliyokwisha toa muongozo.

Nd. Issa alisema viongozi wa kamati za maskuli wanapaswa kufanya juhudi za ziada katika kuwatafuta vijana wa mitaani waliopata  elimu ya kutosha ili watenge muda wa kusaidia masomo ya ziada kwa wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani yao ya taifa.

Katika hafla hiyo waziri wa elimu na mafunzo ya amali zanzibar mh. Riziki pembe juma alikabidhi mashine ya fotokopi kwa skuli ya sekondari ya kitope iliyotolewa na mwakilishi wa jimbo la mahonda balozi seif ali iddi kukamilisha ahadi aliyotoa kwa uongozi wa skuli hiyo miezi michache iliyopita.